–Ataka uwiano wa malipo kati ya watalaam wazawa na kutoka nje
–Mabomba ya mafuta yaendelea kuingia nchini
-Akagua mita za kupimia mafuta Bandari ya Tanga
–Aagiza Bandari ya Tanga na Mtwara zitumike kushusha mafuta kuleta unafuu kwa watumiaji
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka watendaji katika kampuni inayotekeleza mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhakikisha kuwa, Watanzania wanapewa kipaumbele katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ikiwemo ajira na utoaji huduma kama vile ulinzi, chakula, usafiri, bidhaa za ujenzi, huduma za mawasiliano na huduma nyinginezo ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.
Dkt. Biteko amesema hayo mara baada ya kufanya ziara katika Kata ya Chongoleani jijini Tanga na kujionea kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu zikiendelea katika eneo hilo ambalo mafuta kutoka nchini Uganda yatakuwa yakipokelewa na kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Bendera na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
“Serikali inataka kuona watanzania wengi zaidi wanapewa kipaumbele cha ajira katika hatua zote za mradi na hii inajumuisha kampuni za Watanzania zinazotoa huduma mbalimbali, kwa kada ambazo ujuzi wake unapatikana ndani ya nchi, watanzania wapatiwe nafasi na kwa kada ambazo zinahitaji wataalam wa nje lazima kuwe uwiano wa malipo kati ya wazawa na wageni,”amesisitiza Dkt. Biteko
Kuhusu ujuzi unaotolewa na kampuni ya EACOP kwa watanzania wakiwemo kutoka vijiji vinavyozunguka mradi, Dkt. Biteko ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatoa ujuzi ambao ni endelevu utakaowawezesha kuendelea na kazi hata pale mradi utakapokamilika akitolea mfano kuwawezesha kupata mashine za uchomeleaji ambapo ametaka Halmashauri zishirikiane na kampuni ili kutekeleza suala hilo.
Akizungumzia utekelezaji mradi wa bomba la mafuta ghafi litakalokuwa na urefu wa kilomita 1,443 amesema kuwa, unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 32 na mabomba yatakayopitisha mafuta yanaendelea kuingia nchini kwa ajili ya kuwekewa mifumo ya upashaji joto na plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba hayo katika kiwanda kilichopo Sojo wilayani Nzega.
Ameeleza kuwa, ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha mkuza wa bomba umekamilika, kambi za ujenzi zimekamilika na kazi mbalimbali zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa gati katika kata ya Chongoleani mkoani Tanga ambapo meli zitakuwa zikipakia mafuta tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi.
Amesema kuwa, Serikali inayo kiu ya kuwaletea maendeleo Watanzania na ikiamua kutekeleza jambo inafanya bila ulegevu wowote, akieleza kuwa, Tanzania imeshatoa zaidi Dola za Marekani milioni 240 EACOP kama mwanahisa ambaye ana asilimia 15 kwenye mradi huo na kwamba fedha hizo zimekuwa zikitolewa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekagua eneo mafuta yanapopokelewa katika bandari ya Tanga na kukagua mita za kupimia mafuta (flow meter) ambapo aliridhika kuwa mita hizo zinafanya kazi vizuri na hivyo kuleta ufanisi katika shughuli za upakuaji na upakiaji mafuta katika Bandari ya Tanga.
Amesema kuwa, baada ya kurekebishwa kwa kanuni za mafuta, Serikali imeshaagiza mafuta yote ya Ukanda wa Kaskazini yachukuliwe jijini Tanga pamoja na yale yanayoenda nchi za nje kama vile Kenya na mafuta ya Ukanda wa Kusini yachukuliwe bandari ya Mtwara.
Kutokana na hilo, ameziagiza Taasisi zinazosimamia mafuta ikiwemo EWURA, PBPA, TBS na TPA, kufanyia kazi haraka agizo hilo la Serikali kwani kanuni tayari zilishasainiwa kwa ajili utekelezaji wa suala hilo ili kuwawezesha watanzania kupata mafuta kwa bei nafuu.
Akiwa jijini Tanga, Dkt. Biteko pia ametembelea eneo la hifadhi ya mafuta ya kampuni ya GBP ambayo inahifadhi mafuta kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya nchi na kuwaeleza wawekezaji hao kuwa, Serikali inathamini uwekezaji huo na ipo tayari kuwaunga mkono katika mipango yao ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Bendera, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa mradi wa EACOP utakuza pia mapato ya Mkoa wa Tanga pamoja kipato cha mtu mmoja mmoja.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi