January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waombwa kuungana kupinga ukatili wa kimtandao

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa wanawake na wasichana ndio kundi linaloathirika zaidi na ukatili wa kimtandao kuliko wanaume.

Hivyo ili kukomesha ukatili wa aina yoyote ukiwemo wa kimtandao wadau na Watanzania wameombwa kuungana katika kupinga ukatili kwani Tanzania ukatili haukubaliki.

Hayo yamezungumzwa na Muwezeshaji kutoka Zaina Foundations Neema Ndomne,katika mafunzo kuhusu elimu ya kidijitali kwa wanawake waandishi wa habari yalitofanyika kwa njia ya mtandao( zoom meeting) ikiwa ni kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake dunia yalioandaliwa na shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana na Media Convergence pamoja na Zaina Foundations.

Ndomne, amesema unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni na unaowezeshwa na teknolojia ni aina ya dhuluma ya kijinsia na ubaguzi ambao huwekwa katika nafasi za mtandaoni ikiwa ni pamoja na unyanyasaji,uonevu na picha za ngono.

Amesema unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni nchini Tanzania ni pamoja na ukiukaji wa faragha, ufuatiliaji,kuharibu sifa, unyanyasaji mtandaoni, vitisho vya moja kwa moja na vurugu.

Ambapo wasichana wanalengwa mtandaoni kwa sababu tu ya kuwa ni wachanga na wa kike.

Pia amesema,kwa mujibu wa Plan International katika utafiti uliofanywa mwaka wa 2020, asilimia 51 ya wasichana mtandaoni wameripotiwa kukumbana na aina fulani ya unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni kibinafsi kimataifa.

Aidha amesema ripoti ya Afro Barometer inafahamisha kuwa wanawake barani Afrika hawatumii mtandao kama wanaume wanavyofanya na mahali pengine pengo linaongezeka.

Vilevile amesema,kulingana na utafiti uliofanywa na World Web Foundation, Afrika ina pengo kubwa zaidi la kijinsia katika muunganisho wa intaneti/ mtandao ikiwa ni wastani wa Bara karibu asilimia 50 huku wanawake wakiuacha ulimwengu wa mtandaoni ambao mgawanyiko unaweza kuwa mbaya zaidi.

Hivyo hali hiyo inazuia uhuru,ina mnyima mwanamke kupata fursa zinazotokea mtandaoni ikiwemo za kielimu,kiuchumi,jamii,siasa na nyingine.

“Kama watanzania tusimame,tupigane kwa pamoja katika kuzuia ukatili wa kimtandao hususani kwa wanawake na wasichana,” amesema Ndomne.

Kwa upande wake Muwezeshaji kutoka Media Convergency Brighton Cosan, amesema kutuma picha katika mitandao zinaweza kuharibu kesho yao hivyo wasipige picha ambazo zinaweza kuwa na mapokeo hasi ili kukomesha tatizo la ukatili wa kimtandao.

Hivyo amewaomba waandishi kuendelea kuelimisha jamii hasa watoto wa kike kuacha kupiga picha za utupu na kusambaza katika mitandao kwani ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao unawezekana kuzuilika.

Hata hivyo baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema katika suala la ukatili wa mitandaoni wajitahidi kutoa elimu kwa wasichana zaidi kuhusu elimu ya mitandao na namna inavyoharibu ndoto zao,ili waweze kutumia mitandao kwa ufasaha.

Maria Philipo amesema,kupitia mafunzo hayo amejifunza ni namna gani anaweza kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya ukatili wa mtandao ya kijamii na wanavyopaswa kuwa makini kutumia mitandao hiyo pamoja na kutoa elimu kupitia taaluma yao ya uandishi wa habari.

Anith Bwire amesema,katika kuzuia ukatili wa kimtandao wanapaswa kujitambua na kujifunza zaidi kuhusu faida na hasara za mitandao huku Farida Nchimbi alisema,vyombo vya habari vinatakiwa kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia mtandaoni kwa sababu vina nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe katika jamii.

Muwezeshaji kutoka Zaina Foundations Neema Ndomne, akizungumza katika mafunzo kuhusu elimu ya kidijitali kwa wanawake waandishi wa habari yalitofanyika kwa njia ya mtandao( zoom meeting) ikiwa ni kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake dunia yalioandaliwa na shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana na Media Convergence pamoja na Zaina Foundations.picha na Judith Ferdinand
Muwezeshaji kutoka Media Convergency Brighton Cosan, akizungumza katika mafunzo kuhusu elimu ya kidijitali kwa wanawake waandishi wa habari yalitofanyika kwa njia ya mtandao( zoom meeting) ikiwa ni kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake dunia yalioandaliwa na shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana na Media Convergence pamoja na Zaina Foundations.picha na Judith Ferdinand