May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania wanamatarajio makubwa na Sekta ya Madini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

KATIKA kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika Barani Afrika tarehe 16 hadi 23 Juni ya kila mwaka, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewatembelea na kuzungumza na Watumishi wa Wizara ya Madini Makao Makuu katika maeneo yao ya kazi, jijini Dodoma.

Ziara hiyo fupi iliyofanyika Juni 22, 2023, imelenga kusikiliza changamoto, kero, kupata maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa mtumishi mmoja mmoja wa Idara na Vitengo wizarani ili kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya watumishi kwa maendeleo ya Sekta ya Madini.

Akizungumza katika ziara hiyo, ambayo ameitaja kama Wiki ya kufungua milango, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amewataka watumishi kufahamu matarajio makubwa waliyonayo wananchi kuhusu Sekta ya Madini na hivyo kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi na tija na ili kuiwezesha Sekta ya Madini kubadilisha uchumi wa taifa.

‘’ Jamii ya watanzania inaona kabisa rasilimali madini zinaweza kubadili uchumi wa Tanzania na wanayo matarajo makubwa na Sekta hii. Ni vema tukakidhi malengo hayo kwa asilimia inayotekelezeka,’’ amesisitiza Mbibo.

Aidha, amewaeleza watumishi hao kuwa ziara yake imelenga kusikiliza ili hatimaye kuimarisha mazingira ya kazi na kuondoa changamoto ambazo zinahitaji utatuzi wa haraka kwa lengo la kuongeza motisha na tija ya kazi kwa maendeleo ya Sekta ya Madini, na kuongeza kwamba, changamoto zinazohitaji taratibu zaidi za Kiserikali zitafanyiwa kazi.

Vilevile, mbali ya kuwatembelea watumishi, Mbibo ametoa nafasi kwao kuwasilisha kero, changamoto, maoni na ushauri katika ofisi yake na kueleza kuwa, mlango wake uko wazi kuwapokea watumishi ili kuwasilikiza.

Pia, amezungumzia umuhimu wa watumishi kushiriki katika mazoezi na michezo mbalimbali inayoandaliwa na wizara ili kuimarisha afya zao na kutumia fursa hiyo kumpongeza Mtumishi wa wizara ya Madini mwanamichezo mahiri Hilda Masanche ambaye ameteuliwa katika Kamati ya Ufundi ya CECAFA katika mashindano ya CECAFA ya wasichana chini ya miaka 18. Mbali ya kuwa kwenye kamati hiyo Hilda ni Kocha Msaidizi katika timu za taifa Twiga Stars kwa wachezaji wa chini ya miaka 17 na miaka 20

Pongezi hizo zimetolewa na Mbibo kufuatia mtumishi huyo kuishukuru wizara kwa kumpa fursa na nafasi ya kushiriki katika shughuli za michezo mbalimbali ambapo amekuwa akiliwakilisha taifa.

Wakizungumza wakati wa ziara hiyo wafanyakazi kutoka kada mbalimbali wizarani, wameupongeza uongozi wa wizara kwa kutenga muda wao kuwatembelea katika maeneo yao ikiwemo kuwapatia wasaa wa kusikiliza changamoto, kero na kupokea ushauri na maoni yao.

Mbali ya kuwatembelea watumishi katika maeneo yao ya kazi ili kuwasikiliza, Wizara ya Madini imeweka dawati maalum ili kutoa fursa kwa wageni na watumishi kujifunza kuhusu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na wizara ikiwemo kupatiwa nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo yote yakilenga kuimarisha na kuboresha mazingira ya kazi, hali za watumishi na maendeleo ya sekta ya Madini kwa Ujumla.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huenda Sambamba na Kaulimbiu ambapo mwaka 2023 Kaulimbiu inasema ‘’ Kufanikiwa kwa eneo huru la Biashara Barani Afrika (Acfta) kunahitaji Usimamizi wa Utumishi wa Umma wenye Mtazamo wa Kikanda.