Na Rose Itono,Timesmajira
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde ameitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kuhakikisha watanzania wanatambua thamani na faida za kuwatumia Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi katika ujenzi wa Nyumba zao ili waweze kupata makazi bora
Pia ametoa maagizo manne kwa AQRB likiwepo la kuitaka kufanya tafiti za kina ili kuwatambua wahitimu wa taaluma hizo na kuhakikisha wanasajukiwa mapema kwaajili ya kutoa huduma kwa jamii
Akizungumza kwenye semina endelevu ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hiyo Dar es Salaam Dkt Msonde amesema taaluma ya Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi ni muhinu sana si tu kwa Taasisi za serikaliI bali kwa wananchi wote
” Hakikisheni wananchi wanatambua nini thamani na faida watakayoipata kwa kuwashirikisha wataalamu hao,” amesema Dkt Msonde
Amesema kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ni kubwa hivyo ipo haja ya wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kuendeleza kujengeaana uwezo ili kuleta ufanisi katika utendaji wao wa kazi
Dkt Msonde akizungumzia kuhusu maagizo yake manne mbali na kuhakikisha bodi inafanya tafiti za kina ili kuwatambua wahitimu wa taaluma hizo na kuhakikisha wanasajiliwa mapema kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii pia kuhakikisha wahitimu wa taaluma hiyo wanatambuliwa mapema na kuingizwa kwenye mfumo wa kazi rasmi.
Amesema ndani ya vyuo vyetu kuna wahitimu wengi lakini hawajui nini cha kufanya baada ya kuhitimu bodi fanyeni tafiti za kina ili kuwatambua na kuwasajili hata kwa mfumo wa mafunzo kwa vitendo (internship). Hii itawasaidia kupata uzoefu wa kazi na kujiamini

Aidha ameyataja maagizo mengine kuwa ni kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa wataalamu hao Kwa ajili ya kupata fursa katika soko la ushindani, ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yatakayosaidia kuuza ubunifu wao kwa mataifa mengine.
Dkt. Msonde amewaagiza kuhakikisha wataalamu waliopitishwa na bodi ni wale wenye weledi na uwezo wa kusimamia miradi kwa ubora hata pale wakandarasi wakuu wanapoondoka wao wabaki wakiwa vinara katika kuendeleza miradi hiyo.
Pia ameagiza kutafutwa vyanzo mbadala vya fedha ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu hao yanakuwa endelevu na yenye tija katika kukuza taaluma zao.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Mbunifu Majengo Daniel Matondo, amesema AQRB ilianzishwa rasmi mwaka 2010 kwa lengo la kusimamia, kudhibiti weledi, maadili, na ubora wa huduma zinazotolewa na wataalamu wa sekta hiyo nchini.
Amesema tangu utekelezaji wa majukumu ya bodi uanze mwaka 1998, mafanikio makubwa yamepatikana hadi kufikia Juni 2025, jumla ya wataalamu 1,707 na makampuni 491 wamesajiliwa na bodi hiyo, ikilinganishwa na wataalamu 188 na makampuni 53 mwaka 1998.
“Ni muhimu wataalamu wetu washirikishwe kikamilifu tangu hatua za awali za upangaji wa miradi hadi utekelezaji wake. Hii itasaidia kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa rafiki kwa mazingira na inaendana na changamoto za sasa kama mafuriko, msongamano wa magari na ongezeko la watu mijini,” amesisitiza Mbunifu Majengo Matondo.
Ameeleza kuwa bodi imekuwa ikiendesha Programu ya Mafunzo ya Vitendo kwa wahitimu, ambapo jumla ya wahitimu 1,223 wamenufaika tayari, na wengine 283 wakiendelea na mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa Mbunifu Majengo Matondo, programu hiyo inalenga kuwaandaa wahitimu kwa soko la ajira na kuwaongezea uwezo wa vitendo kabla ya kuanza kujitegemea kitaaluma.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi