April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Tulia azindua ujenzi shule ya wavulana Bunge

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, leo Juni 26, 2025, ameongoza hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Shule ya Wavulana ya Bunge, inayojengwa katika eneo la Kikombo, mkoani Dodoma huku akiahidi kwamba vijana watakaopata nafasi katika shule hiyo watalelewa katika maadili mema Ili kupata viongozi Bora wa baadaye.

Katika hotuba yake mbele ya viongozi wa serikali, wabunge, wadau wa maendeleo na wananchi, Spika Dkt. Tulia alitoa pongezi kwa kila mmoja aliyechangia kufanikisha hatua ya awali ya mradi huo wa kihistoria. 

Alisema shule hiyo inalenga kuwa chimbuko la viongozi wa baadaye, wanaolelewa kwa misingi ya maadili, nidhamu, uzalendo na elimu ya kisayansi.

 “Shule hii si ya kawaida. Ni ndoto ya muda mrefu ya kuwa na taasisi maalumu itakayojenga misingi ya uongozi bora kwa watoto wa kiume, ili kulijenga taifa lenye mwelekeo sahihi,” alisema Spika Tulia kwa msisitizo

Alifichua kuwa fedha za kuanzisha ujenzi huo zimetokana na mchango wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia posho zao, wakionesha mshikamano wa kipekee bila kujali kuwa shule inajengwa Dodoma.

 “Tunawashukuru sana waheshimiwa wabunge kwa moyo wao wa kujitoa. Walichangia bila masharti, kwa nia ya dhati ya kuona elimu inaimarika nchini,” alisema.

Spika Dkt. Tulia aliwahimiza wadau wote wa maendeleo – taasisi binafsi, mashirika ya umma, wananchi, na wafadhili – kuendelea kuchangia ili kufanikisha mradi huo unaotarajiwa kubadili mwelekeo wa elimu ya uongozi nchini.

“Maendeleo ya kweli hayawezi kusukumwa na serikali peke yake. Tunahitaji mshikamano wa vitendo, moyo wa kujitolea, na uzalendo kutoka kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.

Akiainisha manufaa ya muda mrefu ya shule hiyo, Spika alisema taasisi hiyo itazalisha viongozi, wataalamu, na wajasiriamali watakaotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa katika karne hii na zijazo.

> “Tunawaomba wadau waendelee kutuunga mkono kwa hali na mali – iwe kwa fedha, vifaa vya ujenzi, au hata ushauri wa kitaalamu. Hii ni shule ya kizazi kijacho, na mafanikio yake yatakuwa ya taifa zima,” alihitimisha.

Shule ya Wavulana ya Bunge inatarajiwa kuwa taasisi ya mfano nchini, ikiweka mkazo kwenye mafunzo ya uongozi, uzalendo, maadili mema, na ubunifu – dira ya kukuza kizazi chenye maono ya kulijenga taifa.