September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania wametakiwa kulinda anga la mtandao kwa kuzingatia matumizi sahihi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WIZARA ya habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewataka Watanzania kuendelea kuwa vinara kushiriki katika ulinzi wa anga la mtandao kwa kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia ya mtandano ili taifa liendelee kuwa salama wakati wote.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Februari 7,2023 na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Mathew Kundo akizungumza katika maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni yanayokwenda na kaulimbiu isemayo”Wezesha watanzania kwa mtandao salama”.

Mha.Kundo ameeleza  kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa na kutafakari juu ya mtandao salama na kuwataka Watanzania kuwa vinara katika ulinzi wa anga la mtandao ili nchi iendelee kuwa salama

Vilevile amewataka wadau wa mitandao kuhakikisha anga la mtandao linakuwa salama kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewezesha fedha za kusimamia na kuratibu anga la mtandao salama.

“Katika miaka ya  hivi  karibuni kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya mawasiliano hapa nchini hadi Septemba 2022 idadi ya watumiaji wa mtandao walikuwa ni milioni 31.1 kwani Tanzania mtandao umekuwa ukipatikana kwa gharama nafuu kuliko nchi nyingine,”ameeleza.

Aidha amesema kuwa Serikali imejipanga kuandaa mazingira bora na wezeshi yanayowezesha utoaji huduma za jamii, kuzalisha ajira na kuongeza pato la taifa na kuongeza uwazi na hata katika uchakataji ajira,

Amesema  kuwa maendeleo yoyote ya teknolojia huja na faida zake na huwa na changamoto mbalimbali za usalama ikiwemo utapeli, unyanyasaji wa kijinsia na wizi wa utambulisho.

Pamoja na hayo amesema kuwa athari zinazotokana na mitandao zinaongezeka, maudhui potofu, unyanyasaji wa kijinsia ipo haja wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kushirikiana kuhakikisha anga la mtandao ni salama kwa watoto hali itakayowezesha watoto na jamii kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na mtandao.

“Ni lazima kujiandaa nini unakwenda kufanya kwenye mtandao kabla ya kuingia, bila tahadhari utaingia kwenye mambo ambayo hukutarajia, ukifungua Instagram, twitter, facebook utaishia kutukana watu, kunyanyasa watu kifikra”amesema Mha.Kundo

Pia ameeleza  Teknolojia ya internet ilivyoleta mapinduzi ambapo ameeleza kwasasa matumizi ya serikali mtandao unapata huduma za serikali kupitia mtandao, teknolojia imesaidia kurahisisha huduma mbalimbali za kiuchummi na kijamii na mapinduzi yameongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.

Kwaupande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mohamed Hamis Abdullah amesema kuwa kuwepo kwa sera pekee haitoshi kila moja anatakiwa kuhakikisha anatumia mitandao bila kuvunja sheria

“Kwani Serikali imetoa elimu na kuhamasisha matumizi salama ili kubaini madhaifu yaliyopo na kuchukua hatua stahiki ili kuongeza ujuzi na weledi katika kukabiliana na matukio ya kiusalama,”amesema.

Naye Afisa Tehama Mkuu wa  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Irene Kahwili,akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA,Dkt.Jabir Bakari amesema kuwa TCRA imeendelea kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya mtandao kupitia klabu za kidigital pamoja na kuratibu mashindano kwa vijana yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kubaini na kukabili vihatarishi vya usalama