February 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania wakumbushwa kudumisha na kulinda amani

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga ambaye ni Mlezi wa Kwaya ya Wasabato Mbeya Kati amewataka wakazi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla kudumisha na kulinda amani ya nchi yetu kwa kujiepusha na vitendo vya uhalifu.

Kuzaga amesema hayo leo,Februari 07,2025 wakati akizungumza na Wana Kwaya wa Kanisa la Wasabato Mbeya Kati (Mbeya Adventist Church) wakiwa wanarekodi wimbo wao mpya unaozungumzia amani ya Afrika na Tanzania.

Kamanda Kuzaga amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini katika kukemea uovu na kuhubiri yaliyo mema na kupelekea jamii kubadilika kwa kuacha uhalifu na kudumisha amani.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Mbeya Kati Christopher Mkama amempongeza Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha amani ya nchi kupitia vyombo vilivyopo vya ulinzi na usalama.

Mwenyekiti wa Kwaya hiyo Peter Chacha amewataka Watanzania kujifunza kupitia nchi nyingine zenye machafuko na kuwataka kuacha kuchezea amani kwani kwenye amani kunatoa fursa ya kuabudu na kufanya kazi za kujipatia kipato.

Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa amesema kuwa ipo nguvu kubwa ya kuzuia na kutokomeza uhalifu kupitia viongozi wa dini, mapadri, mashekhe na wachungaji kupitia mahubiri ya neno la Mungu.

Kwaya ya Kanisa la Wasabato Mbeya Kati kupitia wimbo wao “Amani” imewakumbushwa Wana Mbeya na Watanzania kwa ujumla kulinda amani ya nchi.