Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Online
WITO umetolewa kwa Watanzania kutumia bidhaa za ngozi, ambazo zimekuwa zikizalishwa na viwanda vya ndani ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya kuwa na uchumi imara unaotegemea viwanda.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa leseni kwa wachunaji wa ngozi kutoka Manispaa za Kinondoni, Temeke na Ilala Ofisa Biashara Mkoa wa Dar es salaam, Thabit Massa amesema kwa sasa bidhaa ya ngozi, zimekuwa zikizalishwa kwa viwango vikubwa kutokana na kuwepo kwa viwanda na uwekezaji mkubwa.
Amesema katika mwaka 2019/20, jumla ya vipande vya ngozi millioni 11.77 vinakadiriwa kuzalishwa huku uzalishaji wa ngozi ukiwa sawa na uvunaji wa asilimia 12.5 kwa ng’ombe, asilimia 28.0 kwa mbuzi na asilimia 29.0 kwa kondoo.
“Wastani wa uzalishaji wa ngozi kwa siku ni vipande 31,000 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha futi za mraba millioni 138.57 kwa mwaka, zenye uwezo wa jozi za viatu 55.42,” amesema.
Massa amesema tasnia ya ngozi kwa sasa imekuwa, ambapo kuna viwanda vitano vinavyosindika ngozi kati ya hivyo vinavyosindika kufikia hatua ya mwisho.
Ametaja viwanda hivyo kuwa ni ACE Leather kilichpo mkoani Morogoro, Leather Industry Ltd Moshi, Himo Tannery and Planters Ltd ambavyo vina uwezo wa kusindika futi mraba za 110,000,15000 na 10,000 kwa siku.
Hata hivyo amesema katika kutambua hilo, Wizara ya Mifugo na Uvivu imefanya tathmini ya ubora wa ngozi katika machinjio yenye wachunaji kwa kutoa mafunzo na kuwapatia leseni.
“Tumefanikiwa kuendesha mafunzo ya wachunaji wa ngozi 432 wa machinjio ya Manispaa za Jiji la Dar es Salaam mwaka huu Januari ambapo leo tunawapatia leseni,” amesema.
Ameongeza; “Wizara imewajengea uwezo wakaguzi na waweka madaraja ya ngozi wa Mkoa wa Dar es salaam, Pwani na Morogoro”.
Amewataka wachunaji kuzingatia mbinu mpya za uchunaji bora za ngozi, huku alisisitiza kuwa wasimamizi wa machinjio kuanzia sasa kutoruhusu mtu asiye na leseni kuingia katika machinjio.
Awali Kaimu Mkurungezi Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Gabriel Bura amesema lengo la kutoa mafunzo na leseni kwa wachunaji ni kuhakikisha bidhaa za ngozi zinaweza kuzalishwa katika viwanda vikubwa.
Amesema kwa sasa viwanda vinahitaji ngozi zenye kukidhi viwango, hivyo kutambulika kwa wachunaji wa ngozi kutasaidia kwa kiasi kikubwa uzalishaji kuongezeka.
“Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 45 hadi 65 ya wachunaji wa ngozi, wamekuwa wakichagia uharibifu wa ngozi hivyo tumeona kundi hili ni muhimu kulipa mafunzo kama haya,” amesema Bura.
Salumu Abdallah ambaye ni mmoja wa wachunaji wa ngozi waliopata leseni, amesema mafunzo aliyoyapata yatamsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya kazi yake kwa viwango vyenye ubora tofauti na awali.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi