May 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania kuchangamkia fursa za biashara Iran

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

TANZANIA imeendelea kuwa na Mahusiano mazuri ya kidiplomasia, utamaduni na Iran kwa Zaidi ya miaka arobaini (40) ambayo inahamasisha watanzania kutumia fursa mbalimbali za biashara na Uwekezaji ambazo zinapatikana katika sekta ya Afya, Viwanda, Kilimo na huduma za wateja nzuri kwa uwezeshaji na unafuu wa uendeshaji.

Hayo yamesemwa Julai 01, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Latifa Khamis kwenye hafla ya Maadhimisho ya siku ya Iran iliyofanyika uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam yaliyoanza Juni 28 – 13 Julai, 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Latifa Khamis amesema Maadhimisho hayo yana lengo la kutangaza fursa za biashara na Uwekezaji zilizopo nchini Iran na Tanzania ambazo zipo katika sekta ya Utalii, elimu, Viwanda pamoja na sekta ya Afya.

‘’TanTrade inaendelea kudumisha Mahusiano ya biashara na Uwekezaji yaliyoanzishwa na Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere pamoja na Rais wa zamani wa Iran Ayatollah Khamenei, katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi zaidi” amesema

Aidha, kwa kutangaza bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji katika viwanda vya ndani ya nchi ili kuchochea uzalishaji na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi, hivyo Watanzania watumie fursa za biashara na Uwekezaji zilizopo nchini Iran ili kuongeza mapato kwa Mfanyabiashara mmoja mmoja pamoja na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla .’’ amesema

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TanTrade Ulingeta Mbamba amesema kuwa Irani kuna fursa za kiutalii, elimu na kilimo hivyo tunaweza kuzalisha mazao pamoja na madini na kupeleka katika soko la Irani, pia ni vyema Watanzania wakachamkia fursa ya biashara na uwekezaji zilizopo nchini huko kwani bidhaa zao zina ubora wa viwango vya juu.

‘’Kwa kipindi hiki cha Sabasaba Iran wamekuja kujitangaza na kuendelea kuunga undugu wa kibiashara na Uwekezaji na Watanzania hivyo nawaasa Watanzania waichukulie hii kama fursa ya kujifunza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora viwango vinavyokubalika Kimataifa, pia Iran ni nchi wezeshi kwa Wafanyabiashara wa viwango vya juu vya kati na vya kawaida’’. amesema

Kwa upande wake Balozi wa Iran nchini Tanzania, Hussein Alvandi Behineh ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TanTrade kwa kupata fursa nzuri ya kushiriki na kuazimisha siku ya Iran katika Maonesho ya 47 ya Sabasaba na kuitangaza nchi yao kwa bidhaa wanazozalisha.

“Tunawaomba Watanzania kutembelea Maonesho ya Sabasaba na kwenye banda letu ili kujionea bidhaa tofauti tofauti zenye ubora, viwango vya kimataifa na waje wajifunze fursa za kibiashara zinazopatika nchini Iran’’ amesema