Na Steven Augustino,Timesmajira Online. Nyasa
MKUU wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Isabela Chilumba amewataka wataalamu na viongozi kuanzia ngazi ya vijiji, kata na halmashauri kusimamia kwa weledi uwazi zoezi la uandikishaji wa uhakika wa wanufaika wapya wa mpango wa uhawilishaji fedha kwenye kaya maskini, unaotekelezwa na serikali kupitia mradi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (TASAF) kipindi cha pili cha kuandika orodha ya wanufaika wanaostahili.
Chilumba ameyasema hayo katika kikao kazi na madiwani na wawezeshaji ambao watashiriki katika zoezi la kutafuta wanufaika wapya wa mpango huo katika kikao kilichofanyika wilayani hapa.
Amesema kikao kazi hiki ni mahsusi kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kipindi cha Pili kwa Viongozi, Watendaji na Wawezeshaji hivyo ofisi yake haitegemei kupata malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi, kwani kazi wanayokwenda kuifanya inalenga kulisaidia taifa kuchochea uchumi kwa wananchi wake.
“Mpango wa kunusuru kaya maskini kipindi cha pili, unawataka viongozi kuutekeleza kwa uaminifu na waadilifu mkubwa, ili kuondokana na malalamiko ya wananchi endapo itatokea watachukuliwa wanufaika wasio na sifa na kuachwa wenye sifa,” amesisitiza.
Kutokana na hali hiyo, Chilumba ametoa wito kwa wataalamu na viongozi hao kusikiliza mafunzo kwa umakini kutoka kwa wawezeshaji, ambayo yatawajengea uwezo utakaowawezesha kutekeleza vyema majukumu katika maeneo yao.
Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo, Salum Mshana kutoka TASAF makao makuu amesema kuwa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu, kitatekelezwa kwenye halmashsuri zote 184 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar na utekelezaji huo utafanyika kwenye vijiji, mitaa na sheiya na kujumuisha maeneo ambayo hayakupata fursa hiyo katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kufanya hivyo mradi umepangwa kuzifikia kaya 1,450,000 zenye zaidi ya wanufaika milioni saba kote nchini, ikiwa ni nyongeza ya kaya 350,000 na kwamba mkazo mkubwa katika kipindi cha pili utawekwa kwenye uwezeshaji kaya zitakazoandikishwa katika mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato, huduma za jamii, kuziboresha zilizopo ili ziweze kutoa huduma bora na kuendeleza rasilismali watoto hususan kwenye upatikanaji wa elimu na afya.
Akizungumzia mradi huo Mratibu wa TASAF wilayani Nyasa, Engribert Turuka amesema utekelezaji wa kunusuru kaya maskini ulianza mwaka 2014 na hadi mwaka 2019, ulikuwa unatekelezwa kwenye vijiji 32 na kupitia mpango huo wanatarajia kuingiza vijiji vipya 52 ambavyo havikuwepo kwenye mpango.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa