Na Na Allawi Kaboyo, Biharamulo
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametoa siku saba kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya Biharamulo waliokusanya fedha na kushindwa kuzipeleka benki wawe wamezipeleka kabla ya hatua kali za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao.
Gaguti ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo lililolenga kujibu hoja za Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo miongoni mwazo ni makusanyo ya fedha zaidi ya shilingi milioni 224 ambazo hazikupelekwa benki.
Amesema kuwa, licha ya halmashauri hiyo kufanya vizuri na kupata hati safi bado suala la ukusanyaji wa mapato ni changamoto ambapo aliongeza kuwa, wapo watendaji ambao wanakusanya fedha, lakini hawazipeleki benki na kupelekea halmashauri kuendelea kuandamwa na mzimu wa kutofikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.
“CAG ametoa hoja mbalimbali kuhusu halmashauri hii na nyingi zinalalia masuala ya fedha, natoa siku saba kwa watendaji ambao wamehusika na kutopelekwa fedha hizi wawe wamezirejesha mara moja na kwenye hili sitanii kabisa tutakuja kuonana wabaya kwenye fedha za umma,”amesema Gaguti.
Aidha, alimemuomba mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuitisha kikao kingine maalumu ambacho kitakuwa na agenda za kuangalia mwenendo mzima wa watumishi ndani ya halmashauri hiyo ili hatua husika ziweze kuchukuliwa pale itakapostahili.
Kwa upande wao madiwani wakichangia kwa nyakati tofauti kwenye hoja za hizo za CAG wameitaka halmashauri kumalizia miradi mbalimbali ambayo wananchi tayari wameshaweka nguvu zao hasa vyumba vya madarasa ili kusaidia watoto kusomea katika mazingira ambayo ni mazuri na salama kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi