Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Dar es Salaam
MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuzungumza na Ustawi wa Jamii ili kumsaidia mama aliyetelekezwa na mzazi mwenzake, ili apata haki yake ambayo ni pamoja na nyumba waliyojenga wakati wanaishi pamoja hapo awali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Jokate Mwegelo jana wakati wakati akizungumza na mama huyo nyumbani kwake Mbagala, kata ya Chamanzi, Wilaya ya Temeke, mkoani Dar es Salaam.
Mwanamke huyo anayejulikana kama Asha Makuka, imedaiwa ametelekezwa kwasababu amemzalia mzazi mwenzie watoto saba wa kike bila kuwa na wakiume. Pamoja na kutekelezwa, mwanamke huyo ana changamoto ya malezi ya mtoto wake ambaye amefanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu akiwa amejifungua baada ya kupata ujauzito akiwa masomoni.
“Kuna mama ametelekezwa na mzazi mwenzake sababu amekuwa akipata watoto wa kike tu, matokeo yake imekua ni changamoto kwa mama huyo kutafuta fedha na kulea watoto wake” alisema Jokate
“Baada ya kupata taarifa kuwa kuna mtoto ambae anafanya mitihani ya kidato cha nne huku akiwa amejifungua, tukajaribu kuangalia nini kimesababisha mtoto huyo kupata ujauzito akiwa na umri mdogo,
sababu ni za kijamii kwamba nyumbani baba hayupo, ameitelekeza familia na mama ndiye mwangaikaji kutafuta chakula lakini pia nyumba ambayo walianza kuijenga, yule Mzee kamfukuza na watoto wake ili aoe mwanamke mwingine atafute mtoto wa kiume” alieleza Katibu Mkuu huyo.
Kuhusu mwanafunzi aliyezaa, Jokate amesema wanaangalia namna ya kumsaidia binti huyo apate makazi mazuri ili kujisitiri yeye na mtoto wake mwenye miezi miwili.
Aidha, Jokate amesema atafanya kikao na mawaziri husika wa sekta ya maendeleo ya jamii, sekta ya afya, lakini pia fedha ili waweze kutoa maelekezo kwa serikali nini kifanyike ili kuisaidia jamii katika changamoto hizo.
Katibu Mkuu huyo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa muongozo wa watoto wanapata changamoto mbalimbali kuruhusiwa kuendelea na masomo shuleni kwani uamuzi huo umewagusa zaidi wanaotokana na kaya zenye changamoto kiuchumi na malezi.
“Tunampongeza Rais Samia kwa uamuzi huo ambao leo mtoto huyu aliyepata ujauzito akiwa shuleni ndoto zake hazijakatishwa, na mimi nampongeza kwa kuonyesha ujasiri lakini pia naupongeza uongozi wa shule kwa kumlea na kumuwekea mazingira wezeshi kuendelea na mitihani yake, haya yote yametokana na maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Watoto wote waliopata changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito wamerudi shuleni wakiwa wanajiamini na kuamini ndoto zile zinaenda kutimizwa” alisema Jokate.
Jokate amesema serikali ya awamu ya sita imeshatoa magari ya dharura (ambulance) 727, ambayo yanakwenda katika halmashauri na majimbo nchi nzima kufanya kazi.
Pia Serikali imepata mafanikio makubwa ambapo katika ripoti iliyotoka ya viashiria vya afya ya mama na mtoto imefanikiwa kupunguza vifo kwa asilimia 80 kazi ambayo imefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani tangu alipokuwa Makamu wa Rais alihimiza masuala ya lishe lakini pia afya ya mzazi na mtoto.
Akiwa katika Mtaa wa Kisewe, Kata ya Chamazi, Wilaya ya Temeke, Jokate amemtembelea binti mwenye mtoto wa miezi miwili aliyetumia fursa iliyoitolewa na Rais Samia ya kuendelea na masomo akiwa mjamzito.
Jokate alisema migogoro ndani ya nyumba isiwe sababu ya kushindwa kutoa malezi ya wazazi wote wawili kwa watoto wao. Katibu Mkuu, amewataka wazazi wote kushirikiana katika malezi ya wototo ili wapate muda kufuatilia na kujua mienendo yao ya kimaadili.
UWT imeahidi kufika kokote nchini wakisikia kuna changamoto, lakini pia mafanikio ambayo yamefikiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Asha Makuka, ameushukuru uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa masomoni, kuendelea na masomo yao huku akimshukuru Jokate kwa kumtelembelea na kusikiliza changamoto zinaziwakabili ambapo amemuomba aendelee kufuatilia changamoto hizo ili haki yake ipatikane.
Wakizungumza kwa pamoja, kwa nyakati tofauti mabinti waliopata watoto wakiwa mashuleni, na kujiendeleza na masomo yao, wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwaruhusu kuendelea na masomo yao lakini pia wamemshukuru Jokate kwa kujitoa kwake kuwatembelea na kuwapa mahitaji mbalimbali ya nyumbani, na kutambua changamoto walizonazo ambazo ameahidi kufanyiwa kazi.
Katibu huyo wa UWT mbali na kusikiliza changamoto za wakazi hao wa Mbagala, pia amewapatia mahitaji mbalimbali ya nyumbani.a
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja