March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watahiniwa 595,816 kuanzia mtihani wa kidato cha nne kesho

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Dar

BARAZA la Mitihani la Tanzania(NECTA) limesema jumla ya watahiniwa 595,816 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, mwaka huu kuanzia kesho Novemba 17 hadi Desemba 5, mwaka huu.

Akizungumza jijiji Dar-es+Salaam Novemba 16,2025 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania(NECTA), Profesa Said Mohamed,amesema mtihani huo ni muhimu katika kujua umahiri wa wanafunzi katika masomo yao.

Amesema mtihani huo unahusisha shule 5,868 za sekondari na vituo 813 vya watahiniwa wa kujitegemea katika maeneo mbalimbali nchini hapa.

“Kati ya watahiniwa waliojiandikisha, 569,914 ni kutoka shule za sekondari huku 25,902 wakiwa ni watahiniwa wa kujitegemea.Idadi hii inaonesha ongezeko la watahiniwa 40,585, sawa na asilimia 7.67, ikilinganishwa na mwaka 2024. Wavulana wanakadiriwa kuwa asilimia 46.68 watahiniwa wa shule huku wasichana wakichukua asilimia 53.32,”amesema.

Amesema idadi ya watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 1,128 na kati yao wenye uoni hafifu ni 860, wasioona 70, uziwi 58, ulemavu wa akili watano na ulemavu wa viungo 135.

Profesa Mohamed amesema mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa hatua ya mabadiliko katika elimu, kwani matokeo yake hutumika katika kupangwa kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo ya kidato cha tano au kujiunga na fani mbalimbali za ufundi na ujuzi.

Pia, matokeo ya mtihani ni muhimu kwa jamii na taifa kwa ujumla, kwani hutumika kuamua mustakabali wa elimu na maendeleo ya kijamii.

Kwa ajili ya kuhakikisha mtihani unafanyika kwa ufanisi, maandalizi ya kiufundi yamekamilika na kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimehakikisha mazingira ya mitihani ni salama, huku mikakati ikitekelezwa ili kudhibiti udanganyifu.

Vilevile, amesema wasimamizi wa mitihani wamepewa mafunzo maalum ya kuhakikisha watahiniwa wanapata haki zao na kwamba mtihani unafanyika kwa utulivu.

Aidha ametoa wito kwa kila mdau kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kuzingatia kanuni za mitihani.

” Wasimamizi wanatakiwa kuhakikisha kuwa mtihani unafanyika kwa weledi na kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa, hususan kwa watahiniwa wenye mahitaji maalum, ambao wanahitaji msaada wa ziada kama vile muda wa ziada na mitihani maalum,” amesema

Sanjari na hayo ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano katika kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu huku wananchi wakisisitizwa kutoa taarifa za udanganyifu kwa vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.