November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu wa afya Tabora wapewa mbinu kuboresha huduma

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WATAALAMU wa afya Mkoani Tabora wamepewa mafunzo yanayolenga kuchochea utendaji kazi wenye tija kwa jamii katika suala zima la utoaji huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma hizo.

Mafunzo hayo ya siku 3 yametolewa hivi karibuni na Maafisa Wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Afya katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini hapa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mwezeshaji Hashim Abdallah kutoka TAMISEMI alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kuanzia ngazi ya halmashauri na mkoa.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo wataalamu hao watafikisha elimu hiyo kwa wataalamu walioko chini yao kupitia muongozo wa mshitiri ili kuwapa mbinu sahihi za utoaji huduma bora kwa wananchi ambao ndiyo walengwa wakuu.  

Hashim alifafanua kuwa katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa serikali imeanzisha mpango wa Prime Vender utakaowezesha kila kituo cha kutolea huduma za afya kinakuwa na dawa zinazotakiwa.

Alibainisha kuwa mpango huo utawezesha kununuliwa dawa na vifaa tiba ambavyo havipo ili kuhakikisha mwananchi anapata huduma stahiki wakati wote katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. 

Alisisitiza kuwa Prime Vendor ni mbinu mpya iliyobuniwa na serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuwatumia wazabuni wateule wa uuzaji wa dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha vinapatikana wakati wote katika maeneo ya kutolea huduma.

Mwezeshaji Hashim alifafanua kuwa mpango huu ni suluhu ya kukabiliana na  changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kukosekana dawa kutoka Bohari ya dawa (MSD).

Aidha aliwataka kufanya mapitio ya mara kwa mara katika stoo zao ili kuangalia dawa zilizopo na muda wake wa kuisha na kuagizwa mapema ili wazipate kwa wakati.

Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Luis Bura alishukuru Wizara kwa kuja na mpango maalumu utakaosaidia kumaliza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa dawa hospitalini.

Aliwataka washiriki kuhakikisha wanaaandika kwenye mbao zao za matangazo za vituo vya kutolea huduma ili kuonesha dawa zilizopo na zilizoisha ili kuwapa uelewa na kuwangezea imani ya kupata huduma stahiki.

Mfamasia wa Mkoa huo Dkt Francis Bundara alisema mafunzo hayo yataleta tija kubwa katika utoaji huduma za afya miongoni mwa jamii, hivyo akatoa wito kwa washiriki wote kwenda kuyatendea kazi ili utendaji wao uwe na tija kubwa.