Na Reuben Kagaruki
TANGU chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 ianze kutolewa nchini, kumekuwa na wasiwasi kuhusiana na usalama wa chanjo hizo.
Wasiwasi wa chanjo hiyo unatokana na upotoshaji ambao umekuwa ukifanywa na watu wakitumia hoja zisizokuwa za kitaalam.
Miongoni mwa watu waliokumbwa hofu na chanjo hiyo ni pamoja na wale wenye magonjwa yasiyoambukiza, hatua ambayo inachangia mwitikio wa watu kupata chanjo kuwa mdogo.
Mwitikio huo mdogo unachangiwa kwa kiasi fulani na ukosefu wa elimu, ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan, anasema kama mtu hana elimu ya kutosha hawezi kujitokeza kupata chanjo.
“Nendeni mkafanye kampeni kubwa kwa watu ili wakubali kuchanja kupunguza vifo. Kupita nyumba kwa nyumba kuchanja watu kwa hiari yao hakutasaidia kama watu hawana elimu,” anasema Rais Samia wakati akizindua Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa ALAT jijini Dodoma juzi.
Anasisitiza kwamba mwananchi wa kawaida hawezi kuona ukubwa wa tatizo la Uviko 19 hadi liwe limemtokea nyumbani kwake. “Nendeni mkafanya kampeni kubwa ili watu wakubali kuchanja tupunguze vifo,” anasema Rais Samia.
Kauli hiyo ya Rais Samia ni ujumbe mzito kwa watalaam wa afya na vyombo vya habari ambavyo ni nyenzo muhimu katika kutoa elimu kwa jamii. Katika makala haya, Mwandishi anaeleza faida ya chanjo Uviko 19 kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza, madhara yanayowanyemelea wasipojanja pamoja na usalama wa chanjo hiyo kama inavyothibitishwa na wataalam wa afya na wale wenye magonjwa hayo.
Usalama wa chanjo
Akianza kwa kueleza usalama wa chanjo ya Uviko 19, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume, anawataka wadau wote nchini kuondoa dhana potofu juu ya chanjo ya ugonjwa huo.
“Mimi napenda niwaondoe hofu wananchi wetu kuhusu chanjo hii. Chanjo hii ni salama na ndiyo chanjo sahihi itakayowezesha mtu yeyeto atakayechoma awe salama na kuondokana na hatari ya kupoteza uhai pindi atakapougua ugojnwa huu,” anasema Dkt. Mfaume na kuongeza;
“Maendeleo yoyote yale katika Taifa lolote lile yanaendana na uwepo wa nguvu kazi yenye afya bora, hivyo tujitokeze kwa wingi kupata chanjo kwa faida ya familia yako na hata Taifa kwa ujumla ni jambo la msingi.”
Kuli ya Dkt. Mfaume inaongezwa nguvu na Mkurugenzi wa Kurugenzi wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tatizo Waane, ambaye anatoa wito kwa watu kujitokeza kuchanja kwa kuwa chanjo hiyo ni sawa tu na chanjo zingine ambazo zinatolewa kwa lengo la kuthibiti athari kubwa za ugonjwa huo.
“Chanjo hizi hazina madhara yoyote ni sawa tu kama chanjo zingine na sisi kama wataalamu tunaendelea kusisitiza watu wachanje kwa wingi ili tuweze kupunguza athari za Uviko- 19,” anasema Dkt. Waane.
Faida za chanjo kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza
Kuhusu hofu ambayo wamekuwa nayo watu wenye magonjwa yasiyoambukiza kuhusiana chanjo ya Uviko-19, kwamba inaweza kuwasababishia madhara zaidi, hofu hiyo inaondolewa na Profesa Deodatus Kakoko wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Shule ya Afya ya Umma) akisema chanjo hiyo haina madhara na haiwezi kuwaathiri kwa namna yoyote.
“Watu wenye maradhi yasiyoambukizwa wakipatwa na Uviko-19 wanakuwa kwenye hatari zaidi kutokana na udhaifu wa kinga yao mwili, hivyo ni vema wakajitokeza kupata chanjo ili iweze kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo,” anasema Profesa Kakoko.
Anatoa wito kwa watu walio na magonjwa yasiyoambukizwa watumie fursa ya kuwepo kwa chanjo, kuchanja kwani itawasaidia kuwalinda wasiweze kuathirika kwa virusi vya Uviko 19 na itawaepusha na hatari ya kifo.
Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Omar Ubuguyu, anasema watu ambao wapo kwenye kundi hatarishi endapo wakipata Uviko 19, ni wale wenye magonjwa yasiyoambukiza.
Anataja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na saratani, magonjwa ya figo ambazo zimeshindwa kufanyakazi, kisukari, shinikizo la juu la damu, afya ya akili, selimundu na mengine yanayofanana na hayo.
“Kundi la watu hawa wanaathirika sana pale wanapopata ugonjwa Uviko 19 bila kuwa wamepata chanjo. Imeonekana mara nyingi wakipa maambukizi ya Uviko 19 sukari inaongezeka.
Kwa sasa imebainika miongoni mwa maeneo ambayo Uviko 19 unaathiri ni maeneo ya udhibiti wa sukari ndani ya mwili na hivyo baadhi ya wagonjwa inaonekana sukari zao zinakwenda juu zaidi kuliko kiwango kinachotarajiwa,” anasema Dkt. Ubuguyu.
Tatizo jingine ni fingo za watu hao kushindwa kufanyakazi pindi wakipata uviko na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Kwa nujibu wa Dkt. Ubuguyu takwimu ambazo zimeonekana hivi karibuni zinaonesha zaidi ya asilimia 70 ya watu waliopata madhara makubwa ya Uviko 19 na ambao waliishia kulazwa au kufariki ni wale ambao walikuwa na magonjwa yasiyoambukiza.
“Takwimu hizo sio za Tanzania tu ni dunia nzima kwa hiyo watu ambao wanajifahamu wana magonjwa yasiyoambukiza wanashauriwa zaidi kwenda kuchanja kwa sababu chanjo inawapunguzia mara nne zaidi hatari ya kupata maambukizi ya Uviko 19,” anasema Dkt. Ubuguyu.
Anasema wenye magonjwa yasiyoambukiza ni lazima wapate chanjo kwa sababu ni kwa ajili ya faida ya afya yao, kwa kuwa inapunguza madhara makubwa na pia kifo, ambacho ni miongozi mwa madhara.
“Lakini sio suala la kufa tu au kulazwa, kwani mara nyingi wagonjwa wa Uviko 19 wameishia kupata matatizo ya kudumu ya mapafu, sukari, figo kushindwa kufanyakazi, kwa hiyo mtu ambaye tayari ana magonjwa yasiyoambukiza akipata magonjwa mengine ya kudumu yakiungana na yale aliyokuwa nayo inampa matatizo zaidi,” anasema na kuongeza;
“Wito wetu ni kwamba watu ambao wana magonjwa yasiyoambukiza tunawashauri wachanje, kwani chanjo ya Uviko 19 ni la msingi kwa ajili ya kulinda afya zao na kuwapunguzia mzigo wa gharama na changamoto nyingi za kimaisha, ambazo wanaweza kuzipata ikilinganishwa na wengine ambao hawana magonjwa hayo.”
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Kisuri Tanzania (TDA), Profesa Kaushik Ramaiya, akitumia takwimu za mwezi Agosti, mwaka huu anasema kati ya wagonjwa wa Uviko 19 waliolazwa hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, wengi walikuwa wenye umri mkubwa na wenye magonjwa yasiyoambukiza.
“Anasema wengi waliokuwa wamepata Uviko 19 walikuwa ni wenye uzito uliopitiliza, kisukari, shinikizo la juu la damu na matatizo ya moyo.
Anafafanua kwamba kuchanja hakuwafanyi watu hao wasiweze kupata Uviko 19, lakini wakipata kiwango cha madhara kinapungua ikilinganishwa na wale ambao hawajachanja.
Kwa upande wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dkt. Ramaiya anasema zaidi ya asilimia 86 ya wagonjwa wa Uviko 19 waliolazwa hospitalini hapo hivi karibuni walikuwa na ugonjwa wa kisukari, zaidi ya asilimia 92 shinikizo la juu la damu, asilimia sita walikuwa na pumu na wengine matatizo ya ini na figo.
Kwa hiyo, anasema ni muhimu kwa watu wenye magonjwa hayo kupata chanjo, kwani hata wakipata Uviko 19 hauwi mkali ikilinganishwa na watu wa kundi hilo ambao hawajapata chanjo.
Mkazi wa Kipunguni B, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, Joyce Andrew, anaungana na wataalam hao wa afya, akitoa ushuhuda wa kile ambacho kilitokea katika familia yake.
Anasema ndugu zake wanne waliugua Uviko 19, kati yao watatu walikuwa na magonjwa yasiyoakuambukiza wote waliishia kupoteza maisha. Anasema anakubaliana na hicho wanachokizungumza wataalam hao wa afya, hivyo anatoa mwito kwa Watanzania hasa wenye magonjwa yasiyoakuambukiza kujitokeza kupata chanjo na kupuuza habari za uputoshaji mitaani.
Mmoja wa wagonjwa wa Kisukari na shinikizo la juu la damu, Adelina Balitazar, mkazi wa Chamazi jijini Dar es Salaam anasema yeye aliamua kupata chanjo ya Uviko 10 baada ya kuhakikisha na mdogo wake ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma kwamba chanjo hiyo haina madhara.
“Siamini kama mdogo kwamba mdogo wangu angeweza kunishawishi nipate chanjo hiyo kama ingekuwa na madhara. Hii inadhihirisha wazi kwamba chanjo ni salama, watu wajitokeze kupata chanjo,” anasema Balitazar.
Anafafanua kwamba tangu apate chanjo hiyo afya yake ipo vizuri na hasikii tishio lolote mwilini mwake, jambo ambalo linamhakikishia kwamba chanjo hiyo ni salama kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza.
Akithibitisha jinsi chanjo hiyo isivyokuwa na madhara, Dkt. Shaban Amon, anasema yeye ana tatizo la shinikizo la juu la damu na ni miongoni mwa waliojitokeza kupata chanjo mwanzoni na afya yake inaendelea vizuri.
“Sasa kama mimi ni daktari wa binadamu nina presha, lakini nimejitokeza kupata chanjo nitamshangaa mgonjwa wangu wenye magonjwa yasiyoambukiza akikataa chanjo kwa madai ina madhara, wakati mimi ninayemtibu nimechanja,” anasema Profesa Amon na kuongeza;
“Ni vizuri wale wenye magonjwa yasiyoambukiza wakaelewa kwamba wakipata Uviko 19 na kulazwa ICU uwezekano wa wao kutoka ni mdogo ikilinganishwa na wale ambao hawana magonjwa hayo,”anasema Dkt,Amon.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Mageuzi yanayofanywa na Rais Samia kwa mashirika ya umma kuongeza tija