February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalam Sekta ya utalii watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,kujituma na kuwa wabunifu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Watendaji na Maafisa Utalii nchini wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, kujituma na ubunifu kuhakikisha Sekta ya Utalii inaboreshwa kwa manufaa ya Taifa.

Hayo yamesemwa leo Februari 22, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) katika Kikao kazi cha wataalamu wa Utalii na Masoko kutoka Idara ya Utalii , Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii kilichofanyika jijini Tanga.

“Nitoe wito kwa washiriki wote wa mafunzo haya kutumia fursa hii adhimu kuhakikisha tunajifunza na kuja na mikakati madhubuti ya kuboresha Sekta ya utalii nchini” amesisitiza Chana.

Aidha, ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha nia ya kuleta mageuzi katika sekta hiyo kupitia programu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania.

“Kwa mara ya kwanza sekta hii imevunja rekodi kwa kufikia watalii 5,360,247 ambapo idadi ya watalii wa Kimataifa imefikia 2,141,895 na watalii wa ndani ni 3,218,352 na mapato yatokanayo na shughuli za utalii yalifikia dola za Marekani bilioni 3.9.” amesema Chana.


Awali, akimkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula aliwataka maafisa Utalii kuyajua mazingira ya maeneo yao ya kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi na watalii wanaotembelea maeneo hayo.

Kitandula amesema kuwa Maafisa Utalii wanatakiwa kujua mahitaji ya wateja wanaowahudumia ili kuongeza fursa za wateja kurudi tena kutalii.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi amesema lengo la mkutano huo ni kuongezeana ujuzi wa namna ya kutangaza kidigitali na kuongeza mazao mapya ya utalii.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya Watendaji na Maafisa Utalii na Masoko kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kiliambatana na mafunzo ikiwemo masuala ya afya ya akili, kutumia mbinu za kisasa katika masoko ya kidijitali na matumizi ya akili mnemba (Al).