January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalam Sekta ya Ujenzi kupewa fursa

Na Siti Said, WUU

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), imesema kuwa itaendelea kubadilishana uzoefu na kuwapatia fursa wataalamu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweza kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkati inayotekelezwa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kikao cha nne cha ushirikiano (hawapo pichani),  kati ya Wizara hiyo na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mkoani Tanga.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Sekta hiyo, Mhandisi Joseph Malongo, mkoani Tanga, katika Kikao cha Ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mhandisi Malongo, amefafanua kuwa wataalamu hao watashirikishwa katika miradi inayoendelea kutekelezwa kama vile Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa madaraja makubwa ikiwemo Wami na Tanzanite ili wataalamu hao nao waweze kunufaika kwa utekelezaji wa miradi hiyo nchini.

Mhandisi kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara (RfB), Rashidi Kalimbaga, akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko huo kwa wajumbe wa Kikao cha nne cha ushirikiano kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mkoani Tanga.

“Tumejiwekea kila mwaka wataalamu wa Sekta hii kutoka pande hizi za Muungano kukaa pamoja, kubadilishana uzoefu, sasa tumeona kuna haja ya wataalamu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nao kushiriki katika miradi hii mikubwa kama ambavyo wenzao wanashiriki”,amesema Malongo.

Aidha, Malongo amebainisha kuwa Kikao hicho pia kimeongelea kuhusu  kurasimisha wataalmu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania (SMT), kufanya kazi pande zote za Muungano bila vikwazo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amour Hamil Bakar, akizungumza na wajumbe walioshiriki kikao cha nne cha ushirikiano (hawapo pichani),  kati ya Wizara yake, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mkoani Tanga.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amour Hamil Bakar, amewataka wajumbe wa mkutano huo kuandaa ratiba ya utekelezaji kwa yale wanayokubaliana ili kurahisisha ufuatiliaji wa makubaliano hayo.

Naye, Mhandisi Moses Lawrence, kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), amezipongeza Serikali hizo mbili kwa kuandaa kikao hicho ambacho kinatoa fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu kwa wataalamu wa pande zote na hatimaye kufikia malengo ya pamoja katika suala la miundombinu nchini.

Mhandisi Fauzia Sinde Hassan, kutoka Wakala wa Barabara Zanzibar, amesema kuwa kikao hicho cha wataalamu wa Sekta ya Ujenzi  kinaleta tija kwani hupelekea kujifunza kwa haraka na kupanua mtandao wa mawasiliano kati yao na hivyo kuleta chachu ya maendeleo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ushirikiano huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo (Wanne kulia waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Sekretariati ya kikao cha nne cha ushirikiano kutoka katika Wizara yake na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mkoani Tanga.

Kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kimehusisha  wataalamu wa Sekta ya Ujenzi kutoka pande hizo mbili za Muungano, ambapo lengo kuu la mkutano huo ni kujadili na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya kisekta na kubaini changamoto zinazokabili Sekta hiyo ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.