Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar
MWANASIASA mkongwe Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Stephen Wassira, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina sababu ya kuchapa fomu kwa ajili ya mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, kwani chama hicho tayari kina mgombea (Rais Samia Suluhu Hassan).
Wassira amesema hayo juzi usiku wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Twende Pamoja kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten, jijini Dar es Salaam.
“Nimesikia baadhi ya watu wanasema fomu ni moja kwa mgombea urais wa CCM, mimi nasema fomu hiyo ni ya nini? Katibu Mkuu (Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi) mwenyewe ataamua kama ana hela ya kuchapa fomu hiyo moja, lakini mimi ushauri wangu kwake hakuna haja hata ya fomu hiyo.”
Aidha, Wassira amesisitiza zaidi akisema; “Sisi katika CCM, hatuna tatizo kubwa, nimesikia baadhi ya wenzagu wanasema mwakani tuchape fomu moja, mimi naona tutagharamika bure kuchapa fomu hiyo. Ya nini?
Sisi tuna mgombea tayari na haruhusiwi kwa hisia, bali kwa utamaduni wa chama chetu. Kwa utamaduni wa chama chetu, ukiwa Rais ukamaliza kipindi chako cha kwanza, unaendelea na kipindi cha pili, ndivyo Katiba inavyosema kuwa ndiye mgombea na hakuna mwana CCM anayesema anataka fomu,” amesisitiza Wassira na kuongeza;
“Kama yupo, labda mwakani tumwambie hazipo fomu , tunataka fomu za nini? tunaenda kwenye Kamati Kuu na mgombea wetu ni yule yule (Samia), tunaenda kusema ndiyo, tunaenda kwenye Halmashauri Kuu tunasema sawa, tunaenda mkutano mkuu tunapiga kura, tumemaliza.”
Amefafanua kwamba wana CCM hawana mpango wa kuchukua fomu kwa utamaduni wao na huo sio wa CCM tu, bali hata vyama vingine.
“Marekani pale mwaka huu wanapiga kura Democratic wana mgombea wao, anaitwa Joe Biden, ana miaka 81 na wengine wanasema wamempima wanaona anasahau, lakini Democratic wanasema huyo huyo anayesahau anasahau, ndiye mgombea wao, anaenda kipindi cha pili na cha mwisho,” amesema na kuongeza;
“Sasa wao wana vipimo vyao vya kupima Rais anayesahau, sisi hatuna Rais anayesahau, tuna Rais ambaye amefanya mambo makubwa ambayo watu wengi wanashangaa, kwa hiyo hakuna sababu ya kuchapa hata hiyo fomu moja.
Inachapwa ya nini? Tumalize gharama bure, maana kuchapa fomu moja ni gharama zaidi kuliko kuchapa fomu nyingi.
Wassira amesema miaka mitatu ya Rais Samia anaiona katika utekelezaji wa Ilani, ikiwemo miradi ya maji, afya elimu ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitatu chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Hakuna kata ambayo haijafikiwa na miradi, tumetatua matatizo ya watu, sasa unauliza unaonaje! Naona tunaelekea kushinda, tuna hoja za kuwaambia Watanzania,” alisema Wassira na kuongeza;
“Na sababu za kutaka kuendelea kuongoza tunazo na wenzetu wanaotaka kututoa nao wana zao, tutazipeleka kwa wananchi wazipimi.”
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa