Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Ukerewe
WASIMAMIZI wa mradi wa ukarabati wa maji Kazilankanda -Murutanga wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, wameombwa kusimamia vizuri mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora.
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia fedha za mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa Mohamed Lukonge,wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo ya uhakiki wa miradi ya maendeleo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.
Ambapo Kamati hiyo imekagua jumla ya miradi sita ikiwemo ya maji Kazilankanda-Murutanga, ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Nakoza na Mumbuga,ujenzi wa Chuo cha ufundi Veta- Muhula,Kituo cha afya Igalla na barabara ya Halmashauri-Airport.
Lukonge amesema lengo la serikali ni kusogeza huduma ya maji karibu ambapo awamu ya sita imedhamiria kumtua ndoo mama kichwani hivyo amewaomba wasimamizi wa mradi hasa RUWASA Wilaya kuhakikisha wanamsimamia vizuri mradi huo.
“Tunakuomba kutekeleza mradi huu kwa wakati,kutekeleza mradi kwa kiwango kinachotakiwa,tuna shida moja Mkuu wa Wilaya unajua miradi ya maji imechezewa sana,sasa niwaombe watu wa Ukerewe huu mradi usichezewe na kwenye pesa za UVIKO-19 Rais ni mkali sana ukidokoa tu na yeye anakudokoa,”amesema Lukonge na kuongeza kuwa
“Mhandisi simamia mradi vizuri wananchi wanachohitaji ni maji,hawahitaji siasa maji yakipatikana watu wakapata maji kwa wakati mtatusaidia na sisi wanasiasa kufanya siasa zetu vizuri,kwaio ni waombe sana wasimamizi hasa wewe Mhandisi na wakandarasi tusaidieni sana ili tunapokwenda 2025 iwe rahisi kwetu na kuendelea kusonga mbele,”.
Msimamizi wa mradi huo wa maji kutoka kampuni ya CONSEL Mhandisi Mashala Maduka,amesema mradi huo unapaswa kukamilika June mwaka huu,lakini kwa namna walivyojipanga watakamilisha mradi huo mapema April.
Ambapo wana ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita za maji 135,000, pamoja na vituo 9 vya kuchotea maji.
“Ni kweli kumekuwa na pesa za miradi zikichezewa lakini kwa upande wetu sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba pesa zote tulizopewa zinafanya kazi katika kitu kilicho na ubora na ndio maana tumekuwa tukipima vifaa tunavyokuwa tunavileta sasa na kupitisha pamoja na kucontrol ubora kwa kila kitu kinachofanyika,”amesema Mhandisi Maduka.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ukerewe Mhandisi Zubeda Said, ameeleza kuwa mradi huo utaimarisha huduma ya maji katika vijiji 20 vinavyopata maji kutoka skimu ya za Kazilankanda na Bukindo -Kagunguli pia wameongeza Kijiji cha Murutanga.
Amesema, gharama za mradi huo ni milioni 429.4, ambao utakamilika June 30 mwaka huu, ambapo vijiji 18 vyenye watu 64,041 vitanufaika na skimu ya Bukindo-Kagunguli huku vijiji 2 vya watu 8,865 watanufaika pia inategemea kuongeza wanufaika wapya wapatao 3,094.
“Mradi huu utasaidia kuimarisha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayosababisgwa kwa matumizi ya maji yasiyo safi na salama pia utasaidia kuimarisha uchumi wa jamii kwa kupunguza muda wa kutafuta maji umbali mrefu hivyo kuwapa muda zaidi wa kufanya shughuli za uzalishaji mali,”amesema.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa Mohamed Lukonge,akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa Chama na serikali wa Wilaya ya Ukerewe, alipofika kutazama maendeleo ya mradi wa maji Kazilankanda-Murutanga,wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo ya uhakiki wa miradi ya maendeleo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand.
Mafundi katika mradi wa ukarabati wa maji Kazilankanda-Murutanga wakiendelea na shughuli ya ujenzi wakati wa ziara ya Wajumbe
wa Kamati ya Siasa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa,ilipo fanya ziara ya kutembelea na
uhakiki wa miradi ya maendeleo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja