May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasichana na wanawake wahamasishwe kujiunga na masomo ya sayansi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kuweka jitihada za kuwahamasisha wasichana na wanawake kuingia katika masomo ya Sayansi ili wapende kusoma masomo ya sayansi ambayo yatawafanya kuwa wabunifu na hatimaye kuwa wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo Februari 11,2023 katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na wanawake ambayo yamelenga kuleta chachu kwa makundi hayo ili nchi iweze kuwa na wanasayansi,wahandisi na wabunifu katika nyanja mbalimbali.

“Suala la wanawake na wasichana ni mtambuka na hivyoyanahitaji ushiriki na mchango wa wadau wote bila kujali kama wapo katika sekta binafsi au sekta ya umma.”amesema Kipanga na kuongeza kuwa

“Sote tunatambua kuwa ujuzi uliojengwa katika misingi ya sayansi ,teknolojia ,uhandisi na Hisabati unachagiza ubunifu na ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali kwa Taifa.”

Kwa mujibu wa Kipanga maadhimisho hayo yana umuhimu wa kipekee kuhamasisha wanawake na wasichana kuunga mkono juhudi za serikali kuendeleza ubunifu wa kisayansi ambao ni nyenzo ya msingi katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Buni ,onesha ,inua ,boresha na endeleza,ambayo inalenga kuhamsisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika Sayansi,teknolojia na ubunifu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Elimu,Teknolojia na Ubunifu Profesa Maulilio Kipanyula amesema,siku hiyo ilianza kuadhimishwa na Umoja wa Mataifa 2015 huku kwa hapa nchini ilianza kuadhimishwa mnamo 2021.

Kwa mujibu wa takwimu za UNESCO,ni asilimia 24 tu ya wasichana wote wanaoenda vyuo vikuu ndiyo wanaosoma masomo ya sayansi,teknlojia,uhandishi na hisabati .

Naye Rais wa Taasisi ya Wahandisi wanawake Mhandisi Dkt.Gemma Kishari Modu amesema,katika chama cha wahandisi kina wanachama wapatao 4000 lakini wanawake ni 300 tu na kwamba kwenye Bodi ya Wahandisi ,wahandisi waliosajiliwa ni kama 30000 hivi lakini wahandisi wanawake ni 4000 tu sawa na asilimia kama 12 tu.

“Kwa  hiyo tunatakiwa kuweka jitihada za ziada ili kuweza kuhakikisha kwamba hilo ‘gap’tunaliziba  kwa kuwahamasisha wasichana kupenda masomo ya sayansi ambayo yatawapeleka kwenye masuala ya Sayansi,Uhandisi,teknlojia na hisabati na kuleta tija kwa Taifa hapo baadaye.” Amesema Mhandisi huyo