September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi watatu ‘TapTap Utoboe’wapewa zawadi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

BENKI ya Exim imehitimisha kampeni yake ya kidijitali iliyofanyika kwa miezi mitatu ya iliyofahamika kama ‘Tap Tap Utoboe’ na kutangaza washindi wa Droo kuu ya mwisho, ambapo mshindi wa kwanza amejishindia gari mpya aina ya Mazda CX-5, mshindi wa pili Bajaj aina ya TVS na mshindi wa tatu amejishindia Pikipiki aina ya Boxer.

Washindi hao ni pamoja na Geofreya Muganyizi, Irene Dominick na Bhavesh Gorecha, ambao walipatikana kupitia droo ya mwisho iliyofanyika makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam mapema Septemba 13, 2024 chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, huku ikielezwa lengo la kampeni hiyo kuwa ni kuhamasisha wateja wa Benki ya Exim, kufanya miamala yao kwa kutumia simu zao za mkononi kupitia mitandao.

Akizungumza mara baada ya kutangaza washindi hao, Mkuu wa Kitengo Cha Wateja Binafsi na Biashara za Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo amesema, tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwezi Juni, zaidi ya wateja 200 wameshindwa zawadi za fedha taslimu, ambapo washindi 10 kila wiki walipata zawadi ya Shilingi 50,000 na washindi 10 kila mwezi walipatiwa Shilingi 100,000 kwa kipindi chote Cha kampeni hiyo.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza washindi wetu wote waliotangulia na zaidi niwapingeze washindi wa Droo yetu kubwa tuliyofanya leo na kama tulivyosema Geofrey Muganyizi aliyesinda gari atawekewa mafuta full tank pamoja na bima kubwa mwaka mzima bure hivyo hivyo kwa msondi wa pili na wa tatu”, amesema Andrew Lyimo.

Akizungumzia zaidi mafanikio ya kampeni hiyo Mkuu wa Kitengo Cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu, amesema kampeni ya ‘ TapTap Utoboe’ imekuwa na matokeo mazuri katika kuongeza uelewa na matumizi ya huduma zetu  za kidijitali.

“Dhumuni kuu ni kuhakikisha mteja wetu anapata huduma zenye ubora kwa wakati popote alipo kwa gharama nafuu”, amesema Kafu.

Kwa upande wake Mkuu wa Njia Mbadala za Kidijitali wa Exim Benki, Silas Matoi, ameelezea umuhimu wa ubunifu wa kidijitali kwa benki hiyo “Ubunifu wa kidijitali ndiyo kiini Cha mkakati wetu wa kuboresha huduma zetu kwa wateja”amesema Matoi.

Kampeni ya ‘Tap Tap Utoboe’ ilikuwa sehemu ya jitihada za Benki hiyo kuhimiza jamii kufanya miamala kwa njia ya kielektroniki, ikiwemo kupitia simu za mkononi na mitandao, sambamba na malengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya kuimarisha matumizi  ya kimfumo wa kifedha wa kidijitali.