November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi wa NMB ‘Bonge la Mpango’ wapatikana

Na Angela Mazula, TimesMajira Online


DROO ya kwanza ya Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde inayoendeshwa na Benki ya NMB iitwayo ‘Bonge la Mpango’, imefanyika jana, ambako washindi 10 wameshinda pesa taslimu na wawili wakijitwalia pikipiki ya tairi tatu aina ya Lifan Cargo.

NMB Bonge la Mpango, inalenga kutambua na kuthamini utamaduni chanya wa wateja kujiwekea akiba, ikiwa ni pamoja na kurejesha sehemu ya faida ya benki hiyo kwa mwaka uliopita, ambako NMB ilipata faida ya zaidi ya Sh. Bilioni 205.

Akizungumza wakati wa droo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Ally Ngingite, aliwataka wateja wa benki hiyo kuendelea kujiwekea akiba mara kwa mara, ili kujishindia zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh. Milioni 550

Ngingite alibanisha , ukiondoa pesa taslimu wanazoshinda wateja wa kila wiki, NMB Bonge la Mpango pia inawawezesha wateja wawili wa kila wiki kushinda pikipiki ya mizigo, gari dogo la mizigo aina ya Tata ‘kirikuu’ na Toyota Fortuner.

“Wito wetu kwao ni kudumsha utamadunii wa kujiwekea akiba, ili kujishindia pesa taslimu, pikipiki aina ya Lifan Cargo, kirikuu na Toyota Fortuner. 

“Ukiweka kuanzia Sh. 100,000 anakuwa na nafasi ya kushinda pesa taslimu, pikipiki ama kirikuu na wale ambao akaunti zao zitakuwa na akiba isiyopungua Sh. Milioni 10, watashindania Toyota Fortuner ya Sh. Mil. 169,” alisema Ngingite.

Naye Ofisa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga, aliipongeza NMB kwa kampeni zilizobeba uwezeshaji kwa wateja, huku akiwahakikishia washiriki kuwa droo hizo zinafuata taratibu zote.

“Sisi kama Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, tunaipongeza Benki ya NMB kwa namna ilivyojikita katika kuanzisha na kuendesha kampeni za namna hii, ambazo sio tu zina uwezeshaji, bali pia zinaimarisha utamaduni chanya wa kuweka akiba.

“Tunawahakikishia wateja wa NMB kuwa droo hizi zinasimamiwa na GBT kwa kufuata taratibu na hakuna ubabaishaji wowote. washindi watapatikana kutokana na bahati zao tu na si vinginevyo, hivyo wawe huru kushiriki na watashinda,” alisema Sengasenga.