November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi 75 wa NMB MastaBata KoteKote wamechomoka na Laki moja kila mmoja na Pikipiki

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 10.5 za droo ya kwanza ya Kampeni ya NMB MastaBata ‘Kote Kote’ zimepata wenyewe mwishoni mwa wiki, ambapo washindi 76 walipatikana, 75 kati yao wakijishindia fedha kiasi cha Sh. Mil. 7.5, huku Asumwisye Stallone akiibuka na zawadi ya bodaboda yenye thamani ya Sh. Mil. 3.

Kampeni hiyo, ambayo inaendeshwa na Benki ya NMB kwa ushirikiano na Mastercard International, ikilenga kuhamasisha matumizi ya NMB Mastercard kufanya malipo, Lipa Mkononi kwa kuskani QR na kufanya malipo mtandaoni huku zawadi mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 350 zitatolewa katika miezi mitatu ya kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza kabla ya droo hiyo, Meneja Mwandamizi wa Biashara ya Kadi wa NMB, Manfredy Kayala, alisema malengo makuu ya kampeni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2018, ni kuihamasisha jamii katika kuachana na matumizi ya pesa taslimu ‘cashless’, lakini pia ikilenga kurejesha sehemu ya faida yao kwa wateja wao.

Kayala alifafanua kuwa, ukiondoa bodaboda moja na pesa taslimu kwa washindi 75 wa kila wiki, NMB MastaBata Kote Kote itatoa zawadi kwa washindi 49 wa droo za mwisho wa mwezi, sambamba na bodaboda mbili, na droo ya fainali itazawadia safari za Dubai kwa washindi na wenza wao kwa siku nne.

Mbele ya Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema NMB MastaBata Kote Kote ni muendelezo wa benki yake katika kuwafanya wateja na Watanzania kugeukia utamaduni chanya wa matumizi yasiyohusisha pesa taslimu.

Alifafanua kuwa, MastaBata Kote Kote inagusa wateja wote wa ndani na nje ya nchi wanaotumia kadi za Mastercard au Lipa Mkononi kaa kuscan QR na kutoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanatumia kadi zao katika kufanya malipo na miamala mbalimbali ili kujiweka kwenye nafasi ya kushinda.

Kampeni hii ya NMB MastaBata KoteKote itaendelea kwa takribani miezi mitatu. Kutakuwa na washindi wa kila wiki, kila mwezi na na wale wa Grand Finale.

Wateja wanapaswa kufanya malipo kwa kadi Ya NMB Mastercard au Lipa Mkononi (mastercard QR) ili kujiwekea nafasi ya kushinda.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, akibonyeza kitufe cha kompyuta kuchezesha droo ya kwanza ya Kampeni ya NMB MastaBata ‘Kote Kote’ inayohamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Mlimani City, Deogratius Kawonga na Kulia ni Meneja Mwandamizi Idara ya Kadi na Biashara wa NMB, Manfredy Kayala.