Judith Ferdinand, Mwanza
Wataalamu wa sekta ya ujenzi na uchukuzi,wametakiwa kutumia utaalamu wao kuishauri serikali ili iweze kupata ufanisi katika sekta hiyo.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Rahma Kassim Ali,wakati akifunga mkutano wa nne wa ushirikiano wa watendaji wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Serikali ya Muungano wa Tanzania(SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ),uliofanyika mkoani Mwanza.
Rahma amesema,sekta ya uchukuzi ina umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa na duniani kote,hivyo wataalamu wa sekta hiyo watumie utaalamu wao kuishauri serikali ili iweze kupata ufanisi katika sekta hiyo.
Awali akifungua mkutano huo,Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa.Makame Mbarawa amesema malengo makuu ya Wizara hizo ni kuwa na miundombinu na huduma za uchukuzi zenye ubora na kiwango kinachokubalika kimataifa zilizo salama na zenye gharama nafuu na zinazozingatia uhifadhi wa mazingira.
Prof.Mbarawa amesema,msingi wa utekelezaji wa malengo hayo ni sera,mipango ya kitaifa ikiwemo dira ya taifa ya mwaka 2020-2025 na ile ya mwaka 2020-2050, mipango ya maendeleo ya taifa ya SMT na SMZ,ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na sera za kisekta.
“Nimtumie fursa hii kuwasihi Mwenyekiti na Mwenyekiti Mwenza wa mashirikiano haya, kusimamia vyema kwa umakini utekelezaji wa mipango ilioanishwa kwenye idara hizo,kwa sisi kuhakikisha kwamba tunafikia malengo tuliojiwekea kwa maendeleo ya taifa na wananchi wa Tanzania,”amesema Prof Mbarawa.
Pia amesema,mkutano huo ni muhimu ambao unawasaidia katika shughuli zao,watendaji wakuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi na kutatua changamoto za mashirikiano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ushirikiano huo, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia uchukuzi Gabriel Migire, amesema watafanyia kazi changamoto za kiutendaji.
Pia amesema,washiriki hao walipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya ujenzi iliyotekelezwa na serikali mkoani Mwanza ikiwemo ujenzi wa meli unaoendelea,rada inayotumika kuongezea ndege,daraja la Kigongo -Busisi pamoja na kufanya utalii wa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini