May 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washairi,wadau wa Kiswahili kumuenzi Andanenga(sauti ya kiza)

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online,Dar

Washairi na wadau wa Kiswahili nchini wanatarajia kufanya kongamano la kumuenzi na kukumbuka kazi zilizofanywa na Mshairi nguli marehemu Abdallah Andanenga maarufu sauti ya kiza kuanzia Mei 28 hadi Juni 1,mwaka huu jijini Dar-es-Salaam.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati ya kongamano la kumbukizi ya mshairi nguli huyo, Shekh Hamis Mataka,amesema kutakuwa na shughuli mbalimbali za kumuenzi nguli huyo pia kutakuwa na dua maalumu katika msikiti wa Kinondoni sambamba na kongamano la kifasihi ya lugha ya kiswahili lililoandaliwa na Mfuko wa Fasihi litakalofanyika Makumbusho jijini Dar-es-Salaam.

Amesema pia katika kongamano hilo kutakuwa na midahalo maalumu sambamba na nakala ama kazi mbalimbali zilizotengenezwa na wadau, washairi kama njia ya kumuenzi nguli, fanani ama mtaalamu wa kiswahili na ushairi Tanzania Sheikh Andanenga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Taasisi ya Ukuzaji wa Kiswahili na Ushairi Tanzania ( UKUTA) Hassani Ligile, amesema kuwa marehemu ameacha pengo katika tasnia ya ushairi na kiswahili kwa ujumla.

Amesema Andanenga alikuwa fundi,mahiri na mbobezi wa fani ya ushairi na kiswahili hapa nchini na sehemu zingine duniani ambapo wameandaa machapisho mbalimbali,makala na nyimbo tofauti za kumuenzi gwiji huyo.

Nae Mwenyekiti wa Umoja wa washairi Tanzania ( UWASHATA) Kassimu Pazzi (Amoutile) amesema Andanenga ni mwalimu wake katika fani ya ushairi na kiswahili hivyo akumbukwe kwa kuonesha ukarimu, wake usaidizi na katika ushairi na lugha ya kiswahili hapa nchini.