November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasambazaji,wauzaji dawa za mifugo watakiwa kuzingatia utaratibu wa Serikali

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Dar

WAUZAJI na wasambazaji wa madawa ya mifugo wametakiwa kuzingatia utaratibu ambao umewekwa na Serikali kupitia Baraza la Veterinari Tanzania ili kutoa huduma stahiki kwa wafugaji.

Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli akisisitiza jambo wakati wa kikao kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar es Salaam

Hayo yalisemwa na Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli wakati wa kikao na wauzaji na wasambazaji wa dawa kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa kilichofanyika Jijini Dar es Salaam juzi.

Dkt. Masuruli alisema kuwa bado lipo tatizo kwa baadhi ya wauzaji na wasambazaji wa madawa hayo kutozingatia taratibu ambazo zimewekwa na hivyo kusababisha madhara kwa wafugaji kwa kutopata huduma stahiki.

Baadhi ya wajumbe wa kikao kilichoitishwa na Baraza la Veterinari kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa dawa feki wakisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa wauzaji na wasambazaji wa madawa hayo wanatakiwa kufuata na kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa kuhakikisha madawa yote ya mifugo yanauzwa sehemu ambayo ni sahihi na imesajiliwa na kutambulika na Baraza la Veterinari Tanzania.

Aidha,Dkt. Masuruli aliwahimiza wamiliki hao kuwatumia wataalam wa mifugo katika kutoa huduma hizo kwani kwa kutofanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa wafugaji na hatua zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu zilizowekwa.

Dkt. Masuruli aliendelea kusema kuwa Baraza litaendelea kuwaelimisha wauzaji na wasambazaji wa madawa ya mifugo ili waweze kujua sheria, kanuni na taratibu ili waweze kutoa tiba stahiki kwa wafugaji pale wanapohitaji huduma hiyo.

Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MULTIVET, Dkt. Henry Ruhinguka akihitimisha kikao kilichoitishwa na Baraza la Veterinari Tanzania kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar es Salaam.

Katika kikao hicho wauzaji na wasambazaji wamekubaliana kwa pamoja kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa madawa feki ambayo yamekuwa yakitumiwa na wafugaji kwa kutokujua na kusababisha mifugo yao kutopona na mfugaji kudhoofika kiuchumu.

Naye Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MULTIVET, Dkt. Henry Ruhinguka alisema lipo tatizo la dawa hizo kuuzwa maeneo ya wazi kama minadani ambayo sio sahihi kisheria.

Dkt. Ruhinguka alitumia fursa hiyo kuwahimiza wauzaji na wasambazaji wa madawa hapa nchini kushirikiana na serikali kuhakikisha wanadhibiti tatizo la madawa kuuzwa bila utaratibu unaotakiwa na kuhakikisha wanawadhibiti watu wanaoingiza madawa feki yanayokuja kuleta matatizo kwa wafugaji na kuwarudisha nyuma kiuchumi.