Na Hamisi Miraji, Timesmajira, Online
TIMU ya soka ya Warahibu dawa za kulevya Temeke Mat imefanikiwa kunyakuwa ubingwa wa mashindano ya Warahibu wa Madawa ya kulevya mkoa wa Dar es Salaam.
Katika mashindano hayo, fainali ilifanyika leo kwenye uwanja wa makaburi ya City Makangarawe wilayani Temeke, Timu ya Temeke Mat iliibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Muhimbili Mat.
Magoli ya Temeke Mat yametiwa kimiani na Nico Talu huku goli la pili likifungwa na Omari Ally baada ya kuusindikiza mpira wa krosi.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Temeke Mat ambaye pia mchezaji wa zamani wa Yanga SC na Timu ya Taifa ya Tanzania Seleman Mkati amesema, amefurahishwa sana na ushindi huo kwani aliwandaa vyema vijana baada ya kuonesha vipaji vya hali ya juu.
“Ki ukweli nimefurahi kuona vijana wangu wamefanya kile nilichowaagiza, wameonesha kiwango cha hali ya juu na naamini baada ya mashindano haya, vijana wengi waathirika na madawa ya kulevya watafanya mazoezi ii kuepukana na jangan hilo.
“Kutokana na mashindano haya tutakaa na makocha wenzangu wa Mwananyamala, Mbagala na Muhimbili Mat ili kuteua timu moja ya Warahibu wa madawa ya kulevya tuweze kushiriki Ndondo Cup
“Kupitia sekta ya michezo naamini madawa ya kulevya yatatokomezwa kwani kila mmoja ameona athari zake na sasa hivi wamepokelewa na jamii kutokana na kujiingiza kwenye michezo na kuwa watu safi,” amesema Mkati.
Naye kocha wa Muhimbili Mat Ally Hamad Mbegu amesema, licha ya kukubali kichapo dhidi ya Temeke Mat lakini amefurahishwa na mashindano hayo baada ya kuona Warahibu wa Madawa ya kulevya wakionesha vipaji.
“Mi naungana na Mkati katika kutengeneza timu ya pamoja ili kuwapa hamasa wachezaji kuona walipo ndio chagua sahihi la kutokomeza madawa ya kulevya hapa nchini.
“Niombe Serikali kuwaangalia vijana hawa kwa jicho la upana maana wameamua kuachana na madawa ya kulevya kupitia michezo hivya hawana budi kupewa msaada wa hali na mali ikiwemo kuwawezesha katika vifaa vya mazoezi ambavyo vimekuwa changamoto kwao, lakini pia wadau mbali mbali wajitokeze kuwapa sapoti,” amesema Mbegu.
Kwa upande wake, Nahodha wa Temeke Mat Mussa Hamed Roco amesema, mashindano hayo yamewapa morari mkubwa wa kuachana na madawa ya Kulevya huku akifurahi kuona familia yake wakiungana naye.
“Natoa wito kwa vijana wenzangu ambao wanaendelea na madawa ya kulevya wakiunge na mesadon kwani wataepukana na hali hiyo na kujikuta jamii ikiwakubali. Madawa ya kulevya ni hatari kwa afya ya mwanadamu hivyo tunatakiwa tuyapige vita kupitia michezo tunayoshiriki,” amesema Rico.
Mashindano hayo ya Warahibu wa Madawa ya Kulevya Mkoa wa Dar es Salaam yaliratibiwa na Taasisi ya Kurunzi ya Jamii (KURUJA), ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa na Wizara ya maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum kwa ajili ya kuwapa burudani makundi hayo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania