Na Hamisi Miraji, Timesmajira
Waathirika wa madawa ya kulevya Wilayani Temeke, wameamua kujikita kwenye michezo hasa mchezo wa soka kwa ajili ya kuimarisha afya zao na kutokemeza kabisa uvutaji wa madawa hayo.
Hatua hiyo imekuja, baada ya waathirika hao kukaa pamoja na kutafakari jinsi gani wanaweza kutokomeza uvutaji wa madawa ya kulevya ambayo yamekuwa yakipoteza nguvu ya Taifa.
Akizungumza na Timesmajira leo, mratibu wa waathirika hao Mussa nditi mbwalitate amesema, wameamua kujikita kwenye michezo kutokana na kuimarisha afya za waathirika ili watambue kuwa madawa si kitu kizuri kwa jamii.
“Tumeamua kuanza na mpira wa miguu baada ya kukaa na waathirika kwa pamoja ambapo wengi walipendekeza kuwa wanahitaji kuwa na timu ili waweze kufanya mazoezi.
“Kingine, kujumuika kwa pamoja kubadirisha mawazo huku wakipeana elimu, jinsi gani wanaweza kupambana na kutokomeza kabisa madawa ya kulevya,” amesema Nditi.
Hata hivyo, Nditi ametaja malengo mengine ya kuanzisha timu hiyo kuwa, kubaini na kutambua vipaji ili waweze kuviboresha, kutangaza taasisi bidhaa na uhusiano mwema na jamii na taasisi zingine.
Nditi amesema, tokea wameanza waathirika wengi wamebadilika kutokana na kupenda kufanya mazoezi huku kila mmoja akionesha kipaji chake jambo ambalo limekuwa na faraja.
Hivyo, anahitaji wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kuwapa msaada ikiwemo kupata vifaa vya kufanyia mazoezi kama vile Beeps, Mipira, viatu pamoja na kupata uwanja ambao utakuwa chini yao.
Mbali na hivyo pia amesema, timu hiyo itakapoimarika wanahitaji kucheza michezo ya kirafiki, kushiriki mashindano mbalimbali (bonanza)/ndondo cup.
Naye kocha wa timu hiyo, mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga SC na timu ya Taifa ya Tanzania, Seleman Mkati amewapongeza vijana wengi waliojitokeza kufanya mazoezi kwani amebaini wengi wao wana vipaji vya hali ya juu.
“Ki ukweli hawa jamaa walikuwa wanaelekea kubaya lakini baada ya kujiunga na unywaji wa dawa katika Hospital ya Rufaa ya Temeke, wamekuwa vijana wazuri.
“Lakini pia, baada ya kuwaambia tuanzishe timu kwa ajili ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao kila mmoja alifurahi na kweli hapa mazoezini wanaonekana kuimarika kila siku.
“Tunaiomba Serikali iwaangalie kwa macho mawili ili iweze kuwanusuru kwa kuwapa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezi, nina uhakika kwa kupitia michezo madawa ya kulevya yatatokomezwa,” amesema Mkati.
Timu ya Warahibu wa Madawa ya kulevya Temeke ambao wengi wao wanakunywa dawa katika Hospitali ya Rufaa Wilaya ya Temeke inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Madenge kata ya 14 Temeke.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM