Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Baada ya wadau kuchangia ujenzi wa zahanati mpya ya mtaa wa Bwiru Press wilayani Ilemela mkoani Mwanza Diwani wa Kata ya Pasiansi Rosemary Mayunga ametoa vyeti vya shukrani kwa ajili ya kutambua mchango wao.
Ambapo ametoa vyeti kwa wadau 22,huku akieleza kuwa ujenzi wa zahanati hiyo utakapo kamilika hutahudumia wakazi wasiopungua 8,000 huku Kata hiyo ya Pasiansi ikiwa na idadi ya watu 16,274 wanaume 7,862 na wanawake 8,412 na kaya 4,262 ambao wanategemea huduma ya afya katika zahanati moja.
“Niliona kuna umuhimu wa kutoa vyeti vya shukrani kwa wadau waliounga mkono shughuli za maendeleo ndani ya Kata ya Pasiansi ambao waliochangia ujenzi huu ambao umefikia hatua ya boma kwa kuchanga kiasi cha milioni 38,” amesema Rosemary.
Akizungumza na Timesmajira Online TV Mei 31,2024 Diwani huyo ameeleza kuwa wananchi wa Kata hiyo wamekuwa wakikabiliwa msongamano uliopo katika zahanati ya wema.
Amesema mpango wa kujenga zahanati hiyo ulikuwepo tangu mwaka 2015 baada ya kugundua kuwa zahanati walionayo ya Wema imezidiwa wagonjwa kwani imekuwa inahudumia takribani wakazi wa Kata Tano zilizo jirani na Kata hiyo ya Pasiansi.
“Wananchi ikawa ni shida kupata huduma zinazostahili kwa pamoja na kwa uharaka,ilibidi nichukue fursa ya kubuni mradi huu wa ujenzi wa zahanati mtaa wa Bwiru Press kwa ajili ya kupunguza msongamano kwenye zahanati moja tulionayo ya Wema,”ameeleza Rosemary na kuongeza kuwa:
“Wamekuwa wanapata adha katika zahanati tulionayo sasa hivi,kwanza panatokea upungufu wa watumishi kadhalika dawa zinazoletwa ni kulingana na mahitaji ya idadi ya wakazi wa Kata ya Pasiansi zikawa hazitoshi na baada ya kuhamasisha mitaa yote 8 ya Kata hii na wananchi kuridhia kuwa hilo ni hitaji lao la msingi tulianza mchakato wa kuhamasisha michango mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau wengine ambapo wakasema kila mtaa angalau uchangie milioni 3,”.
Ambapo ameeleza kuwa gharama za ujenzi wa zahanati hiyo mpya kwa bajeti ya serikali na kulingana na mchoro uliopo inahitaji milioni 105 lakini ujenzi wa msingi mpaka boma umegharimu milioni 38 zilizotolewa na wananchi pamoja na wadau wengine.
“Jengo hili tumeisha likabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ili waanze mchakato wa kukamilisha ujenzi huu na kupau na kufanya umaliziaji wa ndani’finishing’, imeonesha nia na kipaumbele cha kukamilisha jengo hili ambapo imeisha tenga kiasi cha milioni 70 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na wananchi waendelee kupata huduma kwa urahisi na wepesi,”.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi huo Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Pasiansi Ally Hassan ameeleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa zahanati ulianza Aprili 15,2023,ikiwa ni utekelezaji wa sera ya serikali ya kuhakikisha kila mtaa unajengwa zahanati au kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya.
Hassan ameeleza kuwa baadhi ya wananchi wa Kata hiyo wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya takribani Kilomita 5 hadi 6,hivyo kupitia ujenzi wa zahanati hiyo mpya utapunguza msongamano wa wagonjwa katika zahanati ya Wema pamoja na umbali wa kufuata huduma katika zahanati hiyo na maeneo mengine.
“Kwa mujibu wa BOQ mpaka jengo la zahanati kukamilika linakadiriwa kutumia kiasia cha milioni 105 na mpaka sasa kiasi cha milioni 38 zimekwisha tumika na kukamilisha ujenzi kwa hatua ya boma ba jamvu kwa michango ya wadau na wananchi,” ameeleza.
Pia Hassan ametaja kuwa kati ya kiasi hicho kilichotolewa na wadau wananchi wamechangia kiasi cha milioni 7.2 pamoja na nguvu kazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula tofali 5,000 yenye thamani ya milioni 6,Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela milioni 5 huku wadau mbalimbali wa maendeleo wakichangia milioni 19.8.
Aidha ameeleza kuwa mradi ulipo fikia wanahitaji nguvu kubwa ya haraka hivyo ameiomba halmy kutoa kipaumbele katika ukamilishaji wa zahanati hiyo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Ilemela Sitta Singibala.kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ameipongeza Kamati ya maendeleo ya Kata hiyo pamoja na wadau waliochangia ujenzi wa zahanati hiyo ambao umefikia hatua ya boma.
Pia ameeleza kuwa changamoto na ombi hilo la ukamilishaji wa ujenzi huo atalifikisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili utekelezaji ufanyike.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu