January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapata mafunzo ya ufugaji kuku na mashine ya kutotolea vifaranga

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Muheza

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ametoa msaada wa mashine ya kutotolea vifaranga vya kuku yenye thamani ya milioni 5, ili iwe mradi kwa wanawake wa Wilaya ya Muheza.

Huku akitoa mafunzo ya ufugaji kuku pamoja na mitungi ya gesi 80 yenye thamani ya milioni 5.6 kwa viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya ya Muheza, Wenyeviti na Makatibu wa CCM kata zote 37 za wilaya hiyo ili kulinda mazingira na kurahisisha maisha.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (wa pili kushoto) akionesha mashine ya kutotolea vifaranga vya kuku kwa wanawake waliohudhuria mafunzo ya ufugaji kuku wilayani Muheza

Ametoa vifaa hivyo kwenye hafla iliyofanyika Mjini Muheza, ambapo ilikwenda sambamba na mafunzo ya ufugaji kuku yaliotolewa kwa viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na CCM ngazi ya kata kwenye Wilaya ya Muheza.

Mhandisi Ulenge amesema anataka kuona wanawake wa Tanga wanakuwa na uchumi mkubwa ambao utawafanya kumudu maisha yao na kusomesha watoto wao, kwani wamezungukwa na fursa nyingi na kinachotakiwa ni utayari ili kuweza kufikia malengo.

“Matamanio yangu kama Mungu alivyoniwezesha ni kuona wanawake wa Tanga tunapiga hatua kwenye shughuli za kiuchumi na maendeleo kama ambavyo anatamani kuona Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan nitafanya liwalo kuona adhima yangu inatimia, na mwanamke wa Tanga anakwenda mbele,” amesema Mhandisi Ulenge.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (kushoto) akimkabidhi mtungi wa gesiMwenyekiti wa CCM Kata ya Masuguru wilayani Muheza, Ismail Sechome

Mhandisi Ulenge amesema wanawake wa Tanga wamekuwa wakisifiwa kwa uwezo wao wa mapishi, sasa imefika mahali, sifa hizo pia zikawe kwenye masuala ya uchumi.

“Baada ya mafanikio mtaweza kuwapa elimu watoto wetu wakinufaika na sisi tumenufaika” amesema Mhandisi Ulenge.

Hata hivyo mashine ya kutotolea vifaranga ina uwezo wa kutotolesha vifaranga zaidi ya elfu moja kwa wakati mmoja na vinatakiwa kugawiwa kwa wanawake wote kwenye kata 37 za Wilaya ya Muheza.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (kulia) akipokea Cheti cha Shukrani kutoka kwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Muheza Theresia Ileti. Ni kwa ajili ya kuwanunulia mashine ya vifaranga na kuwapa mafunzo ya ufugaji kuku wanawake wa Wilaya ya Muheza
Wanawake wa Wilaya ya Muheza wakiwa kwenye Mafunzo ya Ufugaji Kuku