Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wakazi wa Tarafa ya Mwamashimba Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wametakiwa kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuuana kisa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na badala yake malalamiko yao wayafikishe kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.
Ushauri huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa Novemba 23, 2023 alipotembelea Tarafa hiyo ya Mwamashimba kutoa elimu ya Polisi Jamii na kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Polisi Mwamashimba.
Akisikiliza kero kutoka kwa wananchi hao wameeleza kwamba kuna matukio ya mauaji na chanzo kikiwa ni wafugaji ambapo inadaiwa hulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima hivyo migogoro hiyo husababisha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa kushambuliana na kusababisha mauaji.
“Inafikia hatua wafugaji wanachunga ng’ombe zao wakati wa usiku jambo ambalo ni hatarishi sana na wanachungia kwenye mashamba ya wakulima kuna ng’ombe zinaitwa za sheli zinalimishwa asubuhi hadi saa tisa jioni muda wa kupata chakula ni mdogo kwa hiyo usiku zinapelekwa tu kula kwenye mashamba ya watu zinaleta migogoro na kusababisha mauaji,”amesema Hilaly Habibu Sheikh wa Kata ya Mwamashimba.
Akitoa ufafanuzi wa kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi wa Tarafa hiyo, Kamanda Mutafungwa amewataka wakazi hao kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake migogoro yao waifikishe kwenye uongozi ili itafutiwe ufumbuzi.
“Hii migogoro ya ardhi tuipeleke kwa viongozi waitatue na vyombo vingine vipo, itatuliwe kwa masikilizano na maamuzi ya kisheria…..,lakini tukiacha migogoro ya ardhi ikatutawala kama vile hii ardhi tutakufa nayo tutabaki na matatizo ya kuuana na hayataisha, tuache mara moja kujichukulia sheria mkononi,”amesema Mutafungwa.
Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuwafikia wakazi wake popote walipo kwa ajili ya kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya uhalifu kupitia mkakati wake wa kuishirikisha jamii (Polisi Jamii).
Ikumbukwe kuwa, Kituo cha Polisi Mwamashimba kilianza kujengwa Agosti 2023 kwa nguvu za wananchi hadi kukamilika kwake kinatarajiwa kutumia kiasi cha milioni 100 ambapo kwa sasa boma la kituo hicho limeshakamilika huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza akichangia kiasi cha milioni moja kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi