Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
WANUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo kwenye mpango huo, kufanya shughuli ndogo ndogo za kuwaingizia kipato kama kilimo na biashara.
Ili mwisho wa siku, waliojiunga na mpango huo watakapoweza kufuzu (kuweza kujikimu kimaisha) waweze kupisha wengine ambao hawajiwezi na hao waliotoka waweze kuwa na maisha bora na kuwa na kipato cha kati, badala ya kurudi kule kwenye umasikini mkali.
Hayo yamesemwa na Afisa Ufuatiliaji wa TASAF (TMO) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji Korogwe Elizabeth Mwantyala alipotembelea wanufaika hao wakati wa malipo kwenye Mtaa wa Makwei, Halmashauri ya Mji Korogwe.
“Ninachokiomba mjipange kwenye yale mambo yetu kama kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo ili siku ukitoka kwenye huu mradi, basi uweze kusonga mbele badala ya kurudi nyuma,huu mradi una mwisho na hauwezi kuwepo milele, lakini kuna watu ukiwaeleza huwa hawaelewi.
“Kuna mlengwa mmoja nimekuta ana lori mbili za mahindi na gunia mbili za mpunga, lakini anasema tungeendelea endelea sasa ungeendelea hadi lini! unapomueleza wewe umefuzu sasa unatakiwa upishe wenzako wengine waingie kwenye mpango huu, haelewi,lakini nataka kuwaeleza wenzenu wengine wameshatolewa kwenye mpango huu baada ya kufuzu, hivyo na ninyi mjipange” amesema Mwantyala.
Mwantyala amesema Serikali kupitia TASAF, wawezeshaji wametoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanufaika hao, na wengi wao pia wapo kwenye vikundi vya kuweka na kukopeshana, hivyo hayo ndiyo mambo wanatakiwa kuendelea nayo ili wasiweze kurudi nyuma katika shughuli zao za kujiingizia kipato.
Amesema fedha wanazolipwa ilikuwa ni chachu ya kuwawezesha waweze kupata maarifa ya kuweza kujiongezea kipato, kwani kuna baadhi ya wananchi wameweza kutumia fedha za malipo ya TASAF kujenga ama kukarabati nyumba zao, kulima mashamba makubwa na bustani, kununua na kufuga ng’ombe wa maziwa na nyama, mbuzi, kondoo, kuku na bata.
Naye Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara amesema malipo yaliofanyika ni ya miezi ya Mei na Juni, mwaka huu, ambapo malipo ya simu na benki ni sh. 19,177,000.00 kwa kaya 630 na malipo ya fedha taslimu ni sh. 11,096,000 kwa kaya 448 na kufanya
jumla ya kaya zote kwenye halmashauri hiyo zipatazo 1,078 kulipwa sh. 30,273,000.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best