*Yumo mpwa wa marehemu pamoja na mganga wa jadi
*Wamsafirisha kilomita kadhaa mpaka Mwanza kisha kumnyonga
*Mwili wakutwa mwalo wa Ihale-Ilemela
*Chanzo mgogoro wa ardhi machimbo ya dhahabu
Judith Ferdinand na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WATU wanne akiwemo mpwa wa marehemu na mganga wa jadi, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,kwa tuhuma za kuhusika na utekaji na mauaji ya Nestory Marcel (61),mchimbaji wa madini aina ya dhahabu na mkazi wa Stamico Katoro mkoani Geita,kisha kuutupa mwili wake katika mwalo wa Ihale, kando ya Ziwa Victoria wilayani Ilemela mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Naibu Kamishna wa Polisi (DCP),Wilbrod Mutafungwa,amesema hayo Julai 14,2025, wakati akizungumza na waadishi wa habari kuhusiana na mauaji hayo.
Amesema wanawashikilia,Jacob Odhiambo (36),mchimbaji wa madini aina ya dhahabu na mkazi wa Buswelu wilayani Ilemela ambaye ni mpwa wa marehemu huyo,Eric Olang (37),mfanyabiashara na mkazi wa Kishili wilayani Nyamagana pamoja na Abdul Dinisha (29),mkazi wa Taiwan-Nyamhongolo, wilayani Ilemela wakidaiwa kumteka na kumuua Nestory Marcel.
DCP Mutafungwa,amedai kuwa watuhumiwa hao walimteka Marcel huko Katoro, mkoani Geita, wakamsafirisha hadi jijini Mwanza, wakitumia gari aina Subaru Forester,lenye namba T 927 DKW, akiwa chini ya ulinzi wao.
Amesem watuhumwa wakiwa katika barabara ya Igombe kuelekea Kayenze,wilayani Ilemela, walimnyonga shingo (Marcel) ndani ya gari hilo ambalo pia linashikiliwa,kisha walikwenda kuutupa mwili wa wake kando mwa Ziwa Victoria katika mwalo wa Ihale.
“Baada ya kubaini amefariki walikwenda kuutupa mwili wa marehemu majini kwa lengo la kuficha mauaji hayo,kisha walikwenda kwa mganga wa kienyeji,Kulolwa Mbusu (46),mkazi wa Igoma wilayani Nyamagana,kwa lengo la kuoshwa kwa dawa za kienyeji kukwepa wasikamatwe na polisi,” amesema DCP Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Mutafungwa,mwili huo ulionwa na wavuvi ukiwa katika mwalo wa Ihale,Juni 28,2025, majira ya saa 3 asubuhi,wakatoa taarifa kwa polisi ambao walifika eneo hilo kisha kuuchukua.
Pia amesema baada ya mwili wa marehemu Marcel kuchukuliwa na wakati uchunguzi ukiendelea,huko katika Kituo cha Polisi Katoro, ilipokelewa taarifa kuwa Nestory Marcel,alitoweka nyumbani kwake, Juni 23,2025, majira ya saa 12 jioni katika mazingira yasiyoeleweka.
DCP Mutafungwa amesema, uchunguzi wao ulibaini mwili ulipatikana kando ya Ziwa Victoria ni wa marehemu huyo ambaye awali alitambuliwa kwa jinsia yake.Ameeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa umiliki wa ardhi ya machimbo ya dhahabu,kati ya marehemu na watuhumiwa hao huko Rwamgasa Geita.
“Ndugu wa marehemu Nestory baada ya taarifa hizo walifika na kumtambua ikiwemo kupekuliwa maungoni, alikutwa na nyaraka mbalimbali vikiwemo vitambulisho vyake vikimtambulisha kuwa ndiye,” amesema.
Aidha, DCP Mutafungwa ameeleza kuwa, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kukabiliana na mkono wa sheria baada ya upelelezi kukamilika,ambapo jeshi la polisi limeonya wananchi kutojihusisha na matukio ya mauaji,utekaji na uhalifu mwingine.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako