Na Daud Magesa, Timesmajira Online -Mwanza
Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza wakikabiliwa na mashtaka matano ya uhalifu wa kiuchumi ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi noti na utakatishaji wa fedha.
Washtakiwa hao ni Richard Sinkala(38),mkazi wa Buhongwa, Hassan Ibrahim (47), mkazi wa Igoma, Emmanuel Ngama (32), mkazi wa Nyahong’homango na Gerald Majaliwa (30), mkazi wa Buhongwa ,wote ni wakazi wa Mkoaa Mwanza.
Walisomewa mashtaka yao Julai 30, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi, Erick Malrley, huku upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Sileo Mazullah.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza linawahusisha wote wanne kwa tuhuma za kuongoza genge la uhalifu, kinyume na Kifungu cha 4(1), 57(1), na 61(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya 2023).
Shtaka la pili linawahusisha pia wote wanne kwa kosa la kukutwa na noti bandia, kinyume na Kifungu cha 348 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya 2023).
Shtaka la tatu linamhusu mshtakiwa wa kwanza pekee, Richard Sinkala, kwa tuhuma za kughushi noti, kinyume na Kifungu cha 338 cha Kanuni hiyo hiyo.
Shtaka la nne linamhusu Sinkala pia kwa kosa la utakatishaji wa fedha, kinyume na Kifungu cha 12(c) na 13(1)(a) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 423 (Marejeo ya 2023), vikisomwa pamoja na Kifungu cha 57(1) na 61(2) vya Sheria hiyo hiyo.
Shtaka la tano linawahusu washtakiwa wote wanne kwa kosa la utakatishaji wa fedha, wakidaiwa kukiuka masharti ya sheria hiyo hiyo pamoja na Aya ya 22 ya Jedwali la Kwanza la Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Makosa yote yanadaiwa kutendeka kati ya mwezi Januari 2023 hadi Julai 17, 2025 katika maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Mwanza.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Malrley aliwaeleza washtakiwa kwamba hawapaswi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kitakapowasilishwa.
Kwa mujibu wa maagizo ya Mahakama, washtakiwa wote wamerudishwa rumande katika Gereza la Butimba hadi Agosti 13,2025, ambapo kesi hiyo itatajwa tena.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi