November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanging’ombe washukuru kupata hospitali

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Njombe

Hospitali ya Wilaya Wanging’ombe ilipatiwa kiasi cha bilioni 1.3 kutoka serikalini kwa ajili ya majengo na vifaa tiba ambapo kwa sasa hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za upasuaji.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta Novemba 26,mwaka huu wakati alipotembelea kambi ya macho maalum kwa ajili ya matibabu ya mtoto wa jicho yaliyofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Helen Keller International kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya huku akimshukuru Rais kwa kufanikisha kuwa na hospitali ya Wilaya.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe , Claudia Kitta

Amesema hivi sasa huduma mbalimbali zimeanza kutolewa kama kujifungua na wagonjwa wa dharura.

“Kipekee nimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya na sisi kuwa na hospitali ya Wilaya kwani wananchi wengi walikuwa wakienda kutibiwa Ilembula,Njombe na Mbeya ambapo wanatumia gharama kubwa sana,”amesema Kitta.

Ambapo hospitali hiyo imekuwa na majengo ya kisasa na vifaa bora hata kuwezesha matibabu ya kibingwa kufanyika kwa mara ya kwanza Wilaya ya Wanging’ombe.

Kwa upande wake Dkt. Sarah Ludovick Mwakilishi wa Wizara ya Afya amesema Wizara inaendelea kusomesha madaktari wa macho ili huduma za kibingwa ziweze kutolewa wilayani hivyo kuwapunguzia makali wananchi wa kipato cha chini.

Aidha amesema tatizo la mtoto wa jicho ni kubwa nchini ambalo zaidi huwakumba wazee ambao wengi wao hawana kipato na hupoteza uoni na baadhi wamekuwa vipofu.

Naye Dkt. Barnabas Mshangila Daktari Bingwa wa macho kutoka hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya amesema siku tatu za mwanzo wamefanya upasuaji wagonjwa mia moja themanini na tano na wamepata matokeo mazuri.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe , Claudia Kitta,akisalimiana na badhi ya wagonjwa waliopatiwa matibabu ya macho

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Dkt. Frank Chiduo amesema wagonjwa wa mtoto wa jicho katika wilaya yake ni wengi lakini wengi wao hushindwa kufika hospitali kutokana na kukosa fedha za matibabu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya Dkt.Majaliwa Alphonce Chumvi amesema wagonjwa wote wanaopatiwa matibabu hulazwa wodini na hii ni kambi ya kwanza ya mtoto wa jicho kufanyika hospitalini hapo.

Kambi hii itasaidia kuitangaza hospitali kwani wagonjwa wametoka katika kata mbalimbali za wilaya ya Wanging’ombe.

Athuman Tawakal ni Meneja Mradi wa shirika la Helen Keller amesema shirika lake linatoa huduma katika mikoa ya Mbeya,Songwe na Njombe na kambi ya Njombe ni ya kwanza kufanyika lengo ni kuwafikia wagonjwa zaidi ya mia tatu.

“Shirika linawagharamia wagongwa usafiri wa kwenda na kurudi kambi ya matibabu,chakula na gharama zote za matibabu”amesema Athuman.

Ameishukuru serikali pamoja na Wizara ya Afya kwa ushirikiano mzuri hata kuwawezesha kutekeleza majukumu yao bila mkwamo.

Hata hivyo shirika hilo huwajengea uwezo madaktari ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na hata mradi ukiisha muda wake tiba za mtoto wa jicho ziendelee kutolewa lengo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini ambao hawawezi kusafiri wala kugharamia matibabu.

Enock Ngavatula(87)mkazi wa Lugodo ameishukuru serikali kwa kumuwezesha kupatiwa matibabu bure binafsi asingeweza kugharamia matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.

Baadhi ya wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya matibabu ya macho

Ni miaka miwili Enock alipoteza uwezo wa kuona hivyo shughuli za kiuchumi zilikwama na alikuwa mzigo kwa familia kutokana na utegemezi wa kila kitu.

Naye Kundi Masanganya(67)mkazi wa Mbalino Wilaya ya Mbarali amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea hospitali na kuwapatia matibabu ya mtoto wa jicho bila gharama yoyote.