Na Veronica Mrema, Dar es Salaam
WANAWAKE wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo hazina majibu, wengine hawajui pakupata ufumbuzi, hali inayo sababisha baadhi kupatwa magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na unyanyaswaji wa kijinsi na kingono.
Hayo yamebainishwa wakati wa mjadila katika Jukwaa la Women Health Talk 2020 lililowakutanisha wanawake mabingwa kwenye taaluma mbalimbali pamoja na wataalamu mabingwa wa magonjwa ya binadamu ikiwamo ya kina mama, moyo, saratani na kisukari.
Akiwasilisha mada katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Health Promotion Support (THPS), Dkt. Redempta Mbatia amesema wapo baadhi ya wanawake waliowahi kujihusisha na biashara ya kuuza miili lakini sasa wameacha na kujuta kujidhalilisha wenyewe na familia zao.
“Taasisi yetu inafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, tumeshakutana na wanawake 28,000 ambapo 20,000 walikuwa wakijiuza miili yao (dada poa) na theluthi yao wana maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi(VVU),” amesema Mbatia.
“Kwa kundi hili, kiwango cha maambukizi ya Ukimwi ni kikubwa kuliko makundi mengine katika jamii, tabia hii ni hatari inawaingiza katika maambukizi, wengi wao tuliowahoji wamedai wanahitaji kujikwamua kiuchumi,” ameongeza Dkt Mbatia.
Amesema kupitia shirika hilo lililopata ufadhili na kufikia vikundi 250 vya ujasiriamali kila kimoja kina wasichana (young womens) 12.
“Wameanzisha miradi, wanafanya kazi, wengi wanajutia na sasa wameacha tabia hiyo na wengine wamekuwa madiwani katika uchaguzi wa 2020, wapo wanaosikitika kudhalilisha hata watoto wao.”
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Sikudhani Muya ameshauri wanawake kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara. Kwani magonjwa ya saratani yakigundulika mapema ni rahisi kutibika na kupona.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika mkutano huo, Prisca Liymo amsema kuwa mkutano huo umekuja wakati muafaka.
“Pengine mimi ndiye mshiriki mwenye umri mdogo zaidi humu ndani, vijana tuna maswali mengi na hatuna majibu, naomba waandaaji wakati mwingine mtufikirie, mtuandalie jukwaa la kwetu pia, tukutanishwe na wataalamu wa afya, tuulize maswali,” ameomba Prisca.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sophia Byanaku ambaye ni mwanzilishi wa jukwaa hilo, amesema japokuwa yeye si daktarin kitaaluma lakini akiwa kama mhudumu wa afya, amegundua wanawake wanachangamoto nyingi na hawana majibu ya changamoto hizo.
“Niliona vyema nianzishe jukwaa ili kuwakutanisha wanawake na wataalamu ya afya, kwa pamoja tuzungumze ili kupata ufumbuzi katika yale tunayoyapitia,” amesema Byanaku.
Jukwaa hilo linakusudia kuwa endelevu ambapo miaka ijayo linaenga kufikia wanawake na vijana wengi zaidi ili wanufaike na elimu ya afya kutoka kwa wataalamu mabingwa.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia