Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Simanjiro
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT ) Mkoa wa Manyara, Fatuma Tsea, amewataka wanawake kuacha tabia ya kuchafuana hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Tsea ameyasema wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Peter Toima, ya kukagua uhai na kuimarisha chama pamoja na jumuiya zake iliyofanyika wilayani Simanjiro mkoani humo.

Amesema ufike wakati wanawake wapendane na kuheshimiana ili kujenga nidhamu katika Umoja wa Wanawake wa Mkoa huo na sio kuchafuana kuona nani mchafu na nani msafi.
Huku akisisitiza kuwa wanaume wamekua wakifanya uchaguzi kwa staa bila kuchafuana lakini wanawake wanaona ndio sehemu ya kuchafuana ili kumshusha nguvu mwanamke mwenzake asichaguliwe.
“Kipindi hiki ndio cha kujua fulani anatembea na fulani, na yule naye anatembea na fulani, hii ni aibu ni kuchafuana pasipo na sababu ya msingi, kila mtu tunafahamiana hapa hivyo hakuna haja ya kuchafuana,”amesema Tsea.
Sanjari na hayo amewahimiza wanawake wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanaochukua fomu ili kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika nyanja mbalimbali za uongozi.Kwani itambulike uongozi unatoka kwa Mungu, hivyo ni muhimu kwa kila mwanamke anayejiona ana sifa na uwezo wa kugombea ajitokeze kuchukua fomu wakati ukifika.

More Stories
Ilemela yatenga milioni 920 kwa ajili ya mikopo ya vikundi
Tabora Network yawezesha vijana kiuchumi
Serikali Kuboresha Elimu ya Ufundi: Shule 55 Kubadilishwa Kuwa Sekondari za Amali