Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Pwani
WANAWAKE nchini wameombwa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kwenye mpango mpya wa ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ ili waweze kuunganishwa kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi nchini.
Akizungunza na Jukwaa la Kiuchumi la Wanawake Mkoa wa Pwani mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha , Nickson Simon, amesema mpango huo umelenga kuwaunganisha wanawake na fursa za uchumi nchini.
Ameongeza kwamba mpango huo wa ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ ni mkakati rasmi wa Serikali wa awamu ya sita wa kuwainua wanawake kiuchumi na kuwaunganisha na miradi inayoendelea hapa nchini ili waweze kukuza kipato chao.
“Rais Samia Suluhu Hassan amefungua milango ya kiuchumi hapa nchini na fursa mbalimbali kwenye utalii, amevutia wawekezaji na kuboresha miundombinu na ni nafasi ya wanawake sasa kuuunganisha hizo fursa na uchumi wa mtu mmoja mmoja ili kuleta matokeo chanya,” amesisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo ya Kibaha
Amesema Mkoa wa Pwani pekee una takribani viwanda 1, 322 na ni nafasi ya wanawake wa Mkoa wa Pwani na wengineo kuchangamkia fursa zitokanazo na uwepo wa viwanda hivyo kwenye mkoa huo kwa kutoa huduma na kuuza bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais Mambo ya Wanawake na Makundi Maalum, Sophia Mjema alisema mpango huo mpya utawawezesha wanawake kuingia kwenye mfumo mpya wa kieletroniki.
“Nachukua nafasi hii kuwaomba wanawake wa mkoa wa Pwani nyie tumeamua kuanza na nyinyi kwenye program hii ya ‘Imarisha uchumi na Mama Samia’ jisajilini ili Serikali iweze kupata kanzidata na muwe kwenye nafasi ya kusaidiwa.” amesema Mjema
Mjema amesema mpango huo ambao umebuniwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) una dhamira ya kuweza kuwasaidia wanawake nchini nzima kwa kujua hali zao za kiuchumia na mahali wanapofanyia shughuli zao.
Ameongeza kwamba Majukwaa haya ya wanawake yalianzishwa mwaka 2017 na Rais Samia Suluhu Hassana akiwa Makamu wa Rais na lengo kuu ilikuwa ni kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwawezesha kupata mafunzo, elimu ya biashara na mitaji pamoja na mikoipo ili kuendeleza biashara zao na ujasiriamali wao.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Beng’I Issa alisema mpango huo unafungua milango kwa wanawake kutambulika rasmi wao na biashara zao na mahali wanapofanyia shughuli zao za kibiashara.
“Pamoja na mambo mengine mpango huo utaweza kutengeneza kanzidata ya kupata takwimu za wanawake hapa nchini na kuanzia tumeanza na Pwani na tutaendelea nchini nzima,” alisema Bi Issa
Amesema kwamba hizo ni juhudi za Serikali za kuanzisha program hii ambayo itasimamiwa na baraza ili kuweza kuwapa elimu kuhusu mambo ya kodi, biashara , ujasiriamali , kanuni na sheria mbalimbali hapa nchini.
“Biashara nyingi ndogondogo za wanawake asipo rasmi na wengi wenu hamna leseni ila kupitia mpango huu mtakuwa kidogo kidogo kwa kupatiwa mitaji na mikopo kutoka kwenye mifuko na benki za hapa nchini mpaka mtakuwa rasmi,” ameongeza Issa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Kiuchumi la Wanawake Mkoa wa Pwani, Bi Mariam Ulega alisema kwamba atapita wilaya zote za Mkoa wa Pwani ili kuwahamasisha wanawake waweze kujisajili na mpango huo ambao ana uhakika utaleta matokeo chanya.
“Nataka huu Mkoa wetu wa Pwani huo mfano wa kuigwa kwenye program hii kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye usajili na kuanza kuchangamkia fursa hizi ambazo zipo pia katika mkoa huu ili kuweza kujikwamua kwenye umasikini wa kipato,’ amefafanua
‘Tumepokea program hii ‘Imarisha uchumi na Mama Samia’ kwa mikono na natoa rai kwa wanawake wenzangu kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika hili ili tuweze kumuinua mwanamke hapa nchini,’ ameongeza.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato