January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake watahadharishwa kuhusu mahusiano na raia wa kigeni

Na Irene Clemence, Timesmajira Online

MAMLAKA ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imewataadharisha wanawake nchini kuwa makini pindi wanapotaka kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na raia ya wakigeni kwani wamekuwa wakitumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa ajili ya usafirishaji wa dawa hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya DCEA kufanya operesheni katika kipindi Cha miezi miwili na wiki tatu ambapo ilibaini kuwa hiyo ni moja ya mbinu ambayo wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakiitumia kwa ajili ya kusafirisha dawa za kulevya.

Akizungumza Jijini Dar-es-Salaam Juni 19 Kamshina Jenerali wa DCEA, Aretas Lymo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya ukamataji wa dawa za kulevya kupitia operesheni iliyofanyika katika mikoa ya Dar-es-Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha.

Amesema wanawake wanapaswa kuwa makini kwani hali hiyo inaweza kuwasababisha kuingia katika matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku wanaume wakiwakana.

” Asilimia kubwa ya dawa tulizozikamata tumezikuta zikiwa kwa wanawake una mkuta mtu mmoja ana wanawake zaidi ya 2 mpaka watatu na kuficha dawa za kulevya katika makazi yao huku wao wakipanga nyumba tofauti wanakoishi wapenzi wao,”amesema Kamshina Jenerali Lymo.

Ameendelea kueleza kuwa hadi sasa wanawake zaidi 20 wamekamatwa na tayari wapo gerezani kutokana na kukutwa wakiwa wamedhihifadhi dawa hizo ambapo tayari wamefikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.

Hata hivyo aliiasa jamii kuwa makini kwa kutokukubali kupokea mizigo wanayopewa kubeba au kuifadhi pasipo kujua ndani kuna nini.

” Kifungu cha 15 cha sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kinaeleza kwamba ni kosa kusafirisha dawa za kulevya na mtu yoyote atakayethibitika kutenda kosa atawajibishwa kisheria”amesema Kamshina Jenerali Lymo.

Ameeleza kuwa serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii kutokana na kuwepo kwa madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii .

Aidha amesema katika operesheni hiyo DCEA imefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5, bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5465, bangi iliyosindikwa kilogramu 1.5.

Huku methamphetamine gramu 531.43, heroin kete 3878, cocaine kete 138 , mililita 3840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza ekari 1093 za mashamba ya bangi.