November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake wajivunia rekodi ya Rais Samia kwenye sherehe zao

Na Markus Mpangala,TimesmajiraOnline,Dar

DUNIA nzima imetenga siku kadhaa za kuadhimisha kumbukumbu za matukio au mambo mbalimbali.

Serikali za nchi mbalimbali duniani zimesaini makubaliano ya kuheshimu na kuthamini maadhimisho ya siku za Kimataifa.

Dunia inatambua siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka kuwa ni muhimu si kwa wanawake wenyewe bali watu wote Duniani.

Kumbukumbu ya Wanawake Duniani inakusudia kuonesha na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya Dunia. Kuanzia zama za Mapinduzi ya Viwanda hadi teknolojia za kisasa wanawake wametoa michango mbalimbali kupitia sekta binafsi na sekta ya umma.

Vilevile wanawake wametoa michango katika kampuni,serikali,Mabunge,asasi za kiraia pamoja na vyama vya siasa kwa ujumla wake.

Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa wanawake wenye bahati na heshima kubwa kutwaa madaraka ya juu ndani ya nchi yetu. Katika maadhimisho ya siku ya wanawake wana Kila sababu ya kuimba nyimbo za furaha, nderemo na vifijo namna Rais Samia alivyoweka rekodi za aina yake.

Wanawake wa Tanzania wamepitia nyakati mbalimbali za kisiasa na uongozi kuanzia zama za akina Bibi Titi Mohammed hadi Spika wa Bunge Annie Makinda pamoja na umahiri wa uongozi wa mwanamke kama Getrude Mongela ni mifano ambayo wanawake wanatakiwa kutembea kifua mbele na kuona nguvu na maarifa yao yanavyithaminiwa.

Kwa upande wa Rais Samia anazo rekodi nyingi za kusisimua ambazo zinaweza kuwa chachu kwa wanawake kuingia katika siasa na vyombo vya uamuzi.

Mosi, Samia Suluhu Hassan ndiye mwanamke wa kwanza kuliongoza Taifa letu la Tanzania. Kabla ya hapo alishaweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano.

Rekodi hii inaonesha kuwa wanawake wanaweza kutumia majukwaa ya kisiasa kuanzia ndani ya chama, majimbo hadi siasa za Kitaifa. Hili linapaswa kuzingatiwa zaidi kwani wanawake wana kila sababu ya kuthamini nguvu na uwezo wao.

Pili, Samia amekuwa Rais wa tatu mwenye mamlaka ya chama na serikali. Ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa CCM mwanamke.

Bara la Afrika limeshuhudia viongozi wanawake watatu pekee wenye mamlaka ya kuongoza chama na serikali. Joyce Banda ni Rais wa zamani wa Malawi alikuwa Makamu na baada ya kifo cha Bingu wa Mutharika alikabidhiwa jukumu la kuongoza Taifa hilo.

Yeye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama chake cha siasa. Hali kadhalika Rais Elen Johnson Sirleaf alikuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuweka rekodi ya kuwa Rais wa nchi mwenye mamlaka ndani ya chama na serikali nchini Liberia.

Kwa kiasi kikubwa Rais Ellen ndiye aliyeituliza Liberia iloyotoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Rais Samia ameungana na wenzake wawili hao, tofauti na wengine wa kutoka mataifa mengine Afrika ambako Marais wao wanawake hawakuwa na mamlaka kamili ndani ya chama na serikalini.

Tatu, katika uongozi wa Rais Samia umewaka rekodi Afrika Mashariki kuwa ndiye mwanamke wa kwanza mwenye nguvu na ushawishi akiwa Mkuu wa Nchi. Ni sababu hii maelfu ya wananchi wa Kenya wanamtazama Rais Samia kama Shangazi wa Afrika Mashariki.

Jina lake la Suluhu linatumika kama njia ya kuleta amani Afrika Mashariki.

Nne, uongozi wa Rais Samia umeweka rekodi ya kufanya kazi na Spika wa Bunge mwanamke. Ndani ya chama Rais Samia ndiye Mwenyekiti wa CCM na anahusika moja kwa moja katika ushiriki wa mchakato wa kumpata Spika.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina Spika mwanamke, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu ambaye ameweka rekodi ya kufanya kazi na Rais mwanamke mwenzake. Ushahidi huu inaonesha wanawake wana Kila sababu ya kujivunia mafanikio haya na kuhakikisha wanawaombea zaidi.

Tano, vilevile wanawake wanapaswa kutumia mfano wa uongozi wa Rais Samia kuongeza tija ndani ya jamii kuhusu nafasi ya mtoto wa kike. Ni dhahiri wazazi watabadilika kifikra Kwa sababu wanawake wanapata mawazo mapya juu ya ushiriki wao katika masuala ya Uongozi.

Mbele yao kuna wanawake wenye madaraka makubwa na wanafanya maamuzi makubwa kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu. Kila mtoto wa kike anaweza kuwa kama Rais wa iwapo jamii itakubali kuwa wanawake wanayo haki kama walivyo watoto wa kiume.

Sita, Rais Samia ameonesha kuwa inawezekana kupata uongozi wa urithi endapo Katiba ya nchi inaheshimiwa.

Samia anatuma ujumbe kwa wanawake kote nchini kuwa Katiba ni Mali ya wananchi wote bila kujali itikadi, mitazamo, fikra, falsafa au makundi ya kijamii.

Kwamba Katiba inapoheshimiwa inaleta taswira chanya kwa jamii yetu na kwamba wanawake wanapaswa kuamini chombo cha kusimama uongozi kipo na kinatoa fursa sawa Kwa wote kulingana na ngazi wanayotaka.

Saba, katika kuhitimisha, rekodi za Rais Samia zinakwenda kubadili fikra na mitazamo ya wanawake wengi pamoja na wanaume.

Kwani inatarajiwa kushuhudia wimbi la wanawake kuwania nafasi mbalimbali katika chaguzi zijazo. Kwa sababu kiongozi wao wa mfano wameshampata ambaye ni Samia.

Hivyo basi wanawake wanayo fursa na kila sababu ya kujivunia mafanikio haya na kuhakikisha wanatumia mwanya huo kuingia kwenye vyombo vya uamuzi na kuamini inawezekana.