Na Mwandishi wetu
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kutoka Mkoa wa Dodoma, Asia Abdallah, amewataka wanawake wa Kiislamu kutumia elimu ya dini waliyonayo kuelimisha jamii kupitia mitandao ya kijamii, huku wakizingatia stara na maadili ya Kiislamu.
Asia Abdallah ametoa rai hiyo katika hafla ya Maulid ya wanawake iliyofanyika katika Msikiti wa Abdul Aziz, Chang’ombe mkoani Dodoma, ambapo amesema mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya maisha ya sasa na inaweza kutumika kueneza elimu ya dini, kujenga jamii na pia kuwa chanzo cha kipato.
Amesema wanawake wa Kiislamu wanapaswa kuhakikisha wanatumia mitandao kwa mambo yenye manufaa badala ya kuchapisha maudhui yasiyokuwa na ujumbe wa kujenga, akisisitiza kuwa mwanamke anaweza kuwa mtumiaji mzuri wa mitandao bila kuacha misingi ya stara.
“Dunia imehamia mitandaoni. Sidhani kama kuna mtu anaharamisha mitandao, lakini unaweza ukaitumia kwa njia nzuri ikakusaidia wewe, ukajiongezea kipato na pia ukatoa elimu kwa umma,” amesema.
Asia amewataka wanawake wanaosoma Qur’an na wenye elimu ya dini kutumia majukwaa kama Instagram, Facebook, TikTok na mitandao mingine kusambaza elimu hiyo ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Amesema wakati umefika kwa wanawake wa Kiislamu kushindana katika kusoma na kuifahamu Qur’an Tukufu na kutumia elimu hiyo kuwafikia watu wengi, badala ya kushindana katika mambo yasiyokuwa na manufaa kwenye mitandao.
“Wapo wasomaji wengi wa Qur’an humu ndani, lakini ni wangapi wanafikisha elimu hiyo kwa ukubwa wake? Mitandao inaweza kukufikisha kwa watu elfu 10, elfu 30, elfu 80 au hata zaidi, na huwezi kujua ni nani atakayesikia neno lako na likamsaidia,” amesema.
Aidha, amewataka wanawake wa Kiislamu kutumia mitandao kujenga uchumi wao, akisema kuwa matumizi sahihi ya majukwaa hayo yanaweza kuwapatia fursa za kipato kupitia utengenezaji wa maudhui pamoja na fursa nyingine za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Asia Abdallah amewahamasisha wanawake hao kuchangamkia mikopo inayotolewa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Amesema mwanamke anapaswa kuwa na elimu ya dini sambamba na uelewa wa maisha na uchumi, ili aweze kujitegemea na kuimarisha familia na jamii kwa ujumla.
“Mwanamke imara utakuwa imara zaidi kama utakuwa unaijua dini, ukajua na maisha yanavyoenda, lakini ukawa umetengeneza na uchumi,” amesema.
Katika hafla hiyo, Asia Abdallah pia alishiriki katika harambee ya kuchangia ujenzi wa bweni la wanawake, ambapo aliahidi kuchangia Shilingi milioni moja.

More Stories
Range ang’ara riadha BAMATA
NHIF, Aga Khan kuimarisha huduma za saratani Nchini
EWURA yatoa elimu Nishati, Maji maonyesho Geita