December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake Tabora waahidi mitano tena kwa Rais Samia

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

WANAWAKE kutoka taasisi za umma, sekta binafsi, wajasiriamali, wafugaji na wakulima mkoani Tabora wameahidi kumpa kura za kishindo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwakani kutokana na umahiri na kasi ya utendaji kazi.

Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian ambaye sasa kahamishiwa Mkoa wa Tanga amesema kuwa Rais Samia amekuwa neema na baraka kwa wanawake nchini kwani tangu ingie madarakani amefungua milango kwa wanawake wengi kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Hayo ameyaeleza kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8,2024 yaliyofanyika Kimkoa katika uwanja wa Barafu Wilayani Igunga mkoani hapa na kuhudhuriwa na maelfu ya wanawake wakiwemo viongozi mbalimbali.

Amebainisha kuwa ujio wa Rais Samia umefanya nchi kupiga hatua kubwa katika suala zima la kumuinua mwanamke kiuchumi ikiwemo kuaminiwa na kupewa nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali.

‘Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa mama shupavu, makini na Rais wa viwango, anayethamini utu wa mwanamke, ameendelea kuweka mazingira wezeshi kwa akinamama ili kuwainua zaidi kiuchumi,'”amesema.

Dkt Batilda amewataka wanawake wote wa Mkoa huo kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili wawe msaada mkubwa kwa familia zao.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) mkoani hapa Amina Madereka amewataka wanawake wote kutorudi nyuma bali watumie vizuri fursa zote zilizoko mbele yao ili kujikwamua kiuchumi.

Amesisitiza kuwa Rais Samia amewafungulia milango ya masoko ya bidhaa zao hivyo ana uhakika kupitia shughuli zao za ujasiriamali akinamama wa Tanzania watafika mbali zaidi.

Naye Mratibu wa Wajasiriamali na Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa, Ashura Shaban Mwazembe amepongeza serikali kwa kuendelea kulinda haki za wanawake kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Amebainisha kuwa wanawake wa Mkoa huo wamepokea kwa furaha kubwa uamuzi wa Mheshimiwa Rais wa kuanzisha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa kuwa yatachochea kasi ya maendeleo yao.

‘Rais Samia ana dhamira njema ya kuona wanawake wote nchini wanakuwa na maisha bora, katika hili tutaendelea kumuunga mkono na mwakani hatufanyi makosa, tunampa mitano tena,”amesema.

Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta na mwenzake Jackline Kainja wa Viti Maalumu wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwaleta maendele Watanzania.

Wamebainisha kuwa ubunifu wake na juhudi kubwa anazoendelea kufanya ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa utoaji mikopo kwa vikundi vya akinamama, vijana na walemavu ni chachu kubwa ya kuinua maisha ya wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Mkoa huo kupitia CCM, Mwanne Mchemba amesema kuwa wanawake wanajivunia kuwa na Rais Samia kwa kuwa ni mama anayejali maendeleo yao hivyo akawataka kumpa kura zote mwaka 2025.