April 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake Mabogini wajizatiti kuvunja ukimya,usiri vitendo vya ukatili

Na Martha Fatael, Moshi

WANAWAKE Kata ya Mabogini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, wameonesha mfano wa kusherehekea siku ya Mwanamke kwa kujizatiti kuvunja ukimya na usiri unaochangia kuongezeka kwa matukio ya ukatili katika jamii.

Wanawake hao wamefanya maandamano kuanzia hospitali ya Wilaya iliyopo Kijiji Cha Chekereni,ambapo walipanda miti kama ishara ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kudhibiti ukatili wa kijinsia na kushirikiana katika malezi.

Katika tukio hilo, wanawake walisisitiza umuhimu wa kuvunja tabia ya ukimya katika matukio ya ukatili,kushirikiana na kusaidiana, ili kupambana na changamoto zinazozikumba jamii zao.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa kinachoratibiwa na Shirika la kutetea haki na kupinga ukatili wa kijinsia (TGNP),Zainabu Muktazi anasema,kufanya kazi kwa pamoja ni hatua muhimu katika kuzuia ukatili na kuboresha ustawi wa wanawake na watoto katika kata hiyo.

Pia, anahimiza kuwa na ujasiri wa kupaza sauti na kuzungumza kuhusu matatizo yanayohusiana na ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinaonekana na kupewa kipaumbele.

“Tusaidiane wanawake maana kuna ambao wananyanyaswa na hawajui kama ni manyanyaso,wanafanya ni sehemu ya maisha yao,sisi ambao tumepata elimu tunawajibika kuwasaidia wengine kwa kuwapa elimu kuhusu unyanyasaji na athari zake iwapo ukatili huo unafumbiwa macho,”.

Katika hatua nyingine wanawake hao wameiomba serikali kusaidia kukamilisha wodi ya wanawake na watoto hospitali ya Wilaya hiyo,ili kuwarahisishia wanawake hao upatikanaji wa huduma,unafuu na kupunguza gharama na kulea familia zao.

“Asilimia kubwa ya familia za Kata ya Mabogini, zinaendeshwa na wanawake na ndio wazalishaji wakubwa,hivyo wakipunguziwa gharama za hospitali kutawapa nafuu ya maisha,kwani asilimia kubwa ya wanaume wamekimbia majukumu yao na hawataki kazi,” anasema.

Awali Diwani wa Kata hiyo Dkt. Bibiana Massawe, anasema kata hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ingawa mashirika kama TGNP na mengine wakishirikiana na Serikali, yamesaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo, ingawa nguvu zaidi inahitajika katika kutokomeza ukatili.

Anasema natambua mchango wa wengi katika kukabiliana na hali ya ukatili, ingawa jitihada zinapaswa kuongezwa kwa kutoficha taarifa hizo lakini pia jamii kusaidiana pindi matukio kama hayo yanapojitokeza.

Makamu Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Mabogini, Hatangimana Justin, anasema ukatili uliopo katika kata hiyo ni pamoja na wanawake kupigwa na kusababishiwa majeraha makubwa, kufanyishwa kazi kupita kiasi, kutelekezewa majukumu yote ya familia, matusi na udhalilishaji mwingine.

“Tunachohangaika nacho kwa sasa ni kutoa elimu kwa kila njia ikiwemo kwenye mikutano ya kijiji na maeneo mengine, ili wanawake watoe taarifa,waache usiri kwa hofu ya kipigo kwani kuacha kuripoti ndio kunachochea ongezeko la matukio hayo,”.

Anasema ukimya katika matukio ya kikatili, hasa yanapohusiana na ukatili wa kijinsia, unayo athari katika jamii na zinajitokeza katika nyanja mbalimbali ikiwemo ongezeko la matukio hayo.

“Tunaiomba jamii ipaze sauti na isinyamazishwe maana ukimya unaashiria kutozungumza au kutotenda chochote mbele ya vitendo vya ukatili, jambo linalowapa fursa wahalifu kuendelea na vitendo vyao maana wanajua kuwa hakuna atakayewasimamia au kuwaadhibu,” anasema na kuongeza:

“Hivyo matukio ya ukatili yanaendelea kuongezeka na kuchukuliwa kawaida katika jamii,” anasema Justin.

Anasema athari nyingine za usiri wa matukio hayo ni pamoja na kuzuia waathirika wa matukio hayo kupata msaada au kujua njia za kukabiliana na ukatili wanaokutana nao,hivyo inawafanya watu kuwa na hofu na kuhisi kuwa hawawezi kuishi katika mazingira salama, kisaikolojia na kimwili.

“Usiri unaweza kufanya watu kuamini kuwa ni jambo la kawaida kuvumilia vitendo vya ukatili au kunyanyaswa, hivyo inaweza kuchochea tabia za udhalilishaji kwenye vizazi vijavyo, ambapo watoto wanakuwa na mtindo wa kupuuza au kuvumilia vitendo vya kikatili wanapokuwa watu wazima,tunakabiliana nayo kwa kuanzisha klabu za watoto shuleni,”anasema.

Pia anasema ni muhimu kwa vijana kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuzitambua na kuziheshimu haki za wanawake na watoto tangu wakiwa shuleni ili kuongeza wigo wa elimu inayotolewa na kuendelea kupunguza ama kuondokana na matukio haya ya kikatili.

Akizindua siku hiyo ya wanawake, Mbunge wa Viti maalum Ester Maleko anawataka wanawake kutafakari wameweza kupiga hatua kwa kiasi gani katika kukabiliana na ukatili katika jamii na kutetea haki za wanawake na watoto.

“Natamani hapa kila mmoja,tujiulize tumepiga hatua kwa kiwango gani katika kutetea haki za wanawake na watoto, tumetekelezaje kuhusu ukatili wa kijinsia, nadhani tuchukue hatua kila mmoja wetu hapa ili kesho tusigeuke waathirika wa matukio hayo,”anasema na kuongeza:

“Tuache kuwa wa kwanza kutangaza kuhusu watoto wa wengine, wanapopitia changamoto bali tuwasaidie waathirika wa matukio hayo,”.

Pia ameaonya tabia ya baadhi ya wanawake kubeba matukio ya ukatili ya wanawake wenzao ama watoto, kwa kuwasimulia watu wasiohusika ama wasiokuwa na msaada kwa waathirika hao badala yake washikiri kusaidia sheria ichukue mkondo wake ili kuondokana na matukio hayo.

Hata hivyo Mbunge huyo anasema kwa kushirikiana na Wabunge wenzake wataishauri Serikali kuboresha sera na sheria zinazowalinda wanawake ili wanaume waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa haki na ulinzi kwa mwanamke na mtoto.

Akitoa mada kuhusu haki, usawa na uwezeshaji, mjasiriamali Naza Kinyongo, ameitaka jamii kutoa ushirikiano katika kutetea haki kwa wote lakini pia kusimama kwa niaba ya wanawake wengine hususani wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali ili waweze kuwasilisha kero za wanawake kila mara na malengo kufikiwa.