December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WANAVIJIJI 32 WA NDOGOWE NA MILAZO, DODOMA, WAHITIMU MAFUNZO YA UASKARI WANYAMAPORI

Na Mwandishi Wetu, timesmajira

Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) kutoka Kijiji cha Ndogowe na Mlazo, Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma, waliohitimu Mafunzo yao katika Chuo Cha Uhifadhi wa Maliasili Kwa Jamii, wametakiwa Kutumia Kwa weledi Mafunzo waliyopata na si vinginevyo.

Wito huo umetolewa Jana na Mkurugenzi wa Mafunzo, Dkt. Edward Kohi alipokuwa akifunga rasmi Mafunzo ya askari hao katika chuo hicho, Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma na kusisitiza kuwa Mafunzo hayo yamelenga kuwapatia njia rafiki wanavijiji mbinu za kupambana na Wanyama wakali na waharibifu.

Dkt. Kohi amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua umuhimu wa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) katika kuendeleza uhifadhi na kupambana na ujangili nchini kwa kuwa popote ambapo Askari hao wametumika ipasavyo katika shughuli za uhifadhi , wamekuwa wakifanya kazi kwa weledi na mafanikio ya hali ya juu.

Akitoa taarifa ya mafunzo, Mkuu wa Chuo Cha Uhifadhi wa Maliasili Kwa Jamii,Jane Nyau, amesema askari hao 32 wamejifunza mbinu ambazo ni rahisi kuzitumia katika mazingira yao ya kawaida, hazitumii gharama kubwa kiuendeshaji na pia baadhi zinawapatia faida nyingine mbadala.

“Mfano njia ya kutumia mizinga ya nyuki, mbali na kudhibiti wanyamapori hususan tembo, pia wananchi hunufaika kwenye kilimo kwani nyuki hao hao huhusika katika uchavushaji wa maua na hivyo kuwaongezea mazao wakulima”. Anasema

Nyau amesema ni Matumaini ya Chuo kuwa askari hao watakaporejea kwenye maeneo yao wataenda kuwa chachu ya kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kwa kushiriki moja kwa moja katika kuwadhibiti, lakini pia kwa kuwaelimisha wanajamii wenzao kuhusu mbinu mbalimbali ili nao waweze kuzitumia katika kutatua changamoto hii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa timu ya utekelezaji wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya nyara (CPIWT) unaodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP),Damas Masologo,

licha ya kuipongeza jitihada za Chuo hicho, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na Ujangili na Biashara haramu za nyara.