January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaushirika watakiwa kuendeleza ubunifu matumizi ya teknolojia

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira, Online Arusha

WANAUSHIRIKA wa Vyama vya Akiba na Mikopo wameshauriwa kuendelea kujifunza kuhusu Ushirika pamoja na kuendeleza ubunifu na matumizi ya Tehama katika kuboresha huduma za Ushirika kwa wanachama.

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi, Prof. Alfred Sife akiwa mgeni rasmi jana katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Kimataifa ya kuelekea siku ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), Jijini Arusha.

Prof. Sife amesema huu ni wakati kwa wanaushirika kuongeza matumizi ya teknolojia na mifumo ya TEHAMA itakayosaidia kukuza na kuongeza utoaji wa huduma kwa haraka na usahihi zaidi kwa wanachama wa Vyama vya Akiba na Mikopo.

Ameongeza kuwa kufanya hivyo kutaongeza na kuendeleza tija na ufanisi ya utendaji wa vyama hivyo vya Ushirika na kupunguza malalamiko pamoja na vitendo kinyume na taratibu za Ushirika.

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Charles Malunde akieleza utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kusimamia Sekta ya Ushirika nchini wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya kuelekea Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) yaliyoanza Oktoba 12 na kilele chake kkitarajiwa kuwa leo, jijini Arusha. Na mpiga picha wetu.

“Wanaushirika tuboreshe kwa kubuni huduma mpya zinazohitajika kwa wanachama kulingana na mazingira ili tuendane na teknolojia za kisasa zinazoenda na wakati,” amesema Prof. Sife.

Aidha, makamu mkuu huyo alitoa rai kwa Vyama vya Akiba na Mikopo kuendelea kujisajili ili kupata leseni za uendeshaji kwa mujibu wa Sheria Na. 10 ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018) ili kuhakikisha Vyama vinatekeleza majuku yao kwa kufuata Sheria husika.

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Charles Malunde akiongea katika ufunguzi huo amrsema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kutoa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Ushirika inaimarika na kuendelea kutoa mchango katika Pato la Taifa.

“Tume ya Maendeleo ya Ushirika ina wajibu wa kutoa miongozo kwa sekta ya ushirika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013,” alisema Naibu Mrajis Malunde.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) Somoe Nguhwe, amesema maadhimisho hayo mwaka huu ni ya 11 kuadhimishwa hapa nchini kwa kauli mbiu inasema; “Kuchochea matumaini kwa Jumuiya ya Kimataifa”.

Akifafanua Kauli mbiu hiyo inatokana na hali ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa sehemu ya wananchi kupata matumaini ya kiuchumi hususani kwa wananchi wa kipato cha chini.

Aliongeza kuwa vyama hivi vinajiendesha kutokana na mtaji, hisa na akiba zinazotokana na wanachama wenyewe hivyo amewataka Wanaushirika kuzingatia ukopaji wenye tija na urejeshaji kwa wakati.