Na Anthony Ishengoma,Timesmajira Online, Shinyanga
IMEELEZWA kuwa wanaume nchini bado hawajawa na mabadiliko katika kupima afya zao isipokuwa wanapima kupitia wake zao na wamekuwa hawajitokezi kujiunga kwenye vikundi vya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU), hivyo kusababisha kushindwa kumeza dawa za kufubaza virusi kama inavyoshauriwa.
hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Watu Wanaoishi na VVU, Vedasto Mtangila wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanaume Duniani yaliyoadhimishwa mjini hapa.
Mtangila amesema wanaume wanapopima hawawaambii wake zao kuhusu taarifa za afya zao, lakini wao wanataka wanawake wakipima watoe taarifa ili waweze kujua taarifa zao kupitia afya za wake zao.
Amesema hali hiyo inasababisha wanaume kuwapiga hata kuwaua wake zao pale wanapogundua kuwa wanaweke wanatumia ARV na hivyo kuwataka wanaume, waache ukatili dhidi ya wanawake kuhusu dhana zima ya suala la maambukizi ya UKIMWI.
Naye Frank Ernest kutoka Shirika la NACOPHA amesema shirika lake kwa kushirikiana na Mkoa wa Shinyanga, wameandaa maadhimisho hayo mkoani Shinyanga kwa ajili ya kupaza sauti kwa wanaume kuvaa viatu vya akinamama, ili kuyaonja magumu wanayopitia akinamama katika kulea familia.
Ernest amesema maadhimisho hayo, yanafanyika mkoani Shinyanga kutokana na mkoa huo kuwa na takwimu zinazoonesha kuwa asilimia 56 ya wanawake mkoani hapa hawakuwahi kufaidi usichana wao, kwani walitoka utotoni na kuanza maisha ya ndoa.
‘’Ni kwa takwimu hizi ndiyo maana tuko hapa mkoani Shinyanga, kupaza sauti zetu ili wanaume watambue kuwa suala la malezi ya watoto ni jukumu letu sote si la kumuachia mama peke yake na hivyo tuvae viatu vya akinamama, ili tujue magumu wanayopitia katika kulea watoto,” alisema.
Kwa upande wake Meneja Miradi kutoka Shirika la ICS, Sabrina Majikata Meneja amesema ni jukumu la watu wote kumpatia mtoto haki za msingi na kuhakikisha mtoto, anashiriki katika baadhi ya majukumu ya familia lakini si kumtuma mtoto mitaani kufanya biashara, labda kama mtoto atapenda hivyo kwa lengo la kujipatia maarifa.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Ajira na Watu wenye Ulemavu Patrobas Katambi, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo amesema wanaume wanatumika tu katika kukaripia na kutoa adhabu na hivyo kujiweka mbali na upendo wa watoto wao.
‘’Watoto wanapenda mama zao si kwa bahati mbaya ni kwa sababu wako nao muda mwingi, tofauti na wanaume ambao wanatumika tu pale mama anapotaka kuwashtakia kosa na watoto kuwachukulia wanaume kama watu wanaotisha,’’ amesema.
Maadhimisho ya Siku ya Wanaume Duniani yalianza mwaka 1910 kuenzi mchango wa mazazi wa kiume nchini Marekani aliyelea watoto sita peke yake, baada ya mzazi mwenzake kupoteza maisha na kuchukua jukumu la kulea watoto wake kwa kuwapatia haki zote za msingi.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea