December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaokerwa na kelele mtaani, Serikali yatoa mwongozo

Na Lulu Mussa,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)Selemani Jafo amewaagiza wamiliki wa kumbi za starehe na burudani kuhakikisha sauti zitokanazo na shughuli zao hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Saidi Jafo (katikati) akitoa Taarifa kwa Umma ya Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,Dkt. Dorothy Gwajima. Wengine kuanzia kulia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Omary Kipanga jana.

Waziri Jafo amesema hayo hii jana Jijini Dodoma wakati wa kutoa Tamko kwa umma juu ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo na kuwaagiza wamiliki wa maeneo ya burudani na starehe kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti kama ilivyoelekezwa kwenye masharti yote ya leseni zao.

“Katika kuhakikisha tunalinda Afya ya Jamii kutokana na athari zitokanazo na kelele na mitetemo Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; na Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo tunaelekeza Kila Mwananchi ahakikishe shughuli anazofanya hazisababishi kero ya kelele na mitetemo” amesisistiza Jafo.

Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati, Dkt. Franklin Rwezamila, Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt.Thoams Bwana na Afisa kutoka NEMC Makao Makuu,Edgar Mgila wakifuatilia mkutano wa kutoa Taarifa kwa Umma ya Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo jana.

Aidha, Waziri huyo amesema kasi ya ukuaji wa uchumi inaenda sambamba na ongezeko la shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo zinaambatana na ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na Kelele na Mitetemo na kusababisha athari za kiafya na kimazingira kwa jamii.

Ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika Nyanja za kiuchumi na kijamii kutokana na Mipango madhubuti ya Serikali kwenye Uwekezaji katika Sekta mbalimbali.

Hivyo, ameutaka umma wa Watanzania kuhakikisha agenda ya kelele na mitetemo inakuwepo kwenye mikutano ya wakazi na kuwaomba wananchi kutoa taarifa kuhusu kero na mitetemo kwa Ofisi za Serikali za Mitaa au NEMC kwa Namba za bure (0800110115 au 0800110117 au 0800110116)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima akifafanua jambo wakati wa mkutano wa kutoa Taarifa kwa Umma ya Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo

Amesema yeyote atakayesababisha kero zitokanazo na kelele na mitetemo kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa kelele na mitetemo) za mwaka 2015 atakuwa amevunja sheria na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, sambamba na kufungiwa kwa biashara husika.

Kwa upande mwingine Waziri Jafo ametoa rai kwa viongozi wa Dini kupitia Kamati za Amani, kulijadili suala hili la Kelele na Mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha ibada kwa maslahi mapana ya afya ya jamii.

Nae Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima amesema wataendelea kuelemisha jamii juu ya athari za kiafya zitokanazo na kelele na mitetemo iliyopitiliza ili kuwa na jamii yenye afya bora na kupunguza gharama za matibabu kwa Serikali.

Waziri Jafo aliambatana na Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Wenye Ulemavu Ummy Nderiananga, Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Chillo, na Naibu Waziri Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo Pauline Gekul.