January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

SERIKALI mkoani Tabora imeagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizopo katika Mkoa huo,kuwasaka wazazi na walezi watakaobainika kuficha watoto wenye ulemavu ambao wamefikisha umri wa kwenda shule.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS) Dkt.John Mboya alipokuwa akiongea na watendaji, wataalamu na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Akiongea kwa niaba yake Ofisa Msimamizi wa Fedha wa Mkoa huo, Shan Mwangesho, ameeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuficha watoto wenye mahitaji maalumu na kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Hivyo ameagiza,watoto wote waliofikisha umri wa kuanza shule wakiwemo wenye ulemavu wakaandikishwe ili waanze masomo pale shule zitakapofunguliwa,kwani Serikali inataka watoto wote wapate elimu pasipo na kikwazo.

“Wakurugenzi lisimamie hili ipasavyo, haya ni maelekezo ya Mkoa, hakikisheni watoto wote wanapewa fursa ya kupata elimu kokote waliko, atakaye ficha mtoto wake kwa kisingizo chochote iwe ulemavu au sababu nyingine mkamateni”, ameeleza.

Mwangesho amesisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wana haki sawa na wengine na wana uwezo wa kufanya vizuri hata katika masomo yao, hivyo kuwaficha ni kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu na hilo halikubaliki.

“Hakikisheni wanaoficha watoto wanasakwa ili waeleze kwa nini wanawaficha, kama mzazi au mlezi hana uwezo wa kumpeleka shule atoe taarifa ili halmashauri iangalie namna ya kumsaidia kutokana na ulemavu wake,”ameeleza.

Aidha amepongeza halmashauri hiyo kwa kuendelea kuwa kinara wa ukusanyaji mapato katika Mkoa huo, hivyo akazitaka Halmashauri nyingine kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ikiwemo kubuni vyanzo vipya.

Pia ameelekeza Halmashauri zote kuhakikisha zinatumia asilimia 60 ya mapato yao kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 40 kwenye matumizi ya kawaida ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wao.