May 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanandoa,wapenzi waonywa kutopekua simu za wenza wao

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza 

Imeelezwa kuwa tabia ya wanandoa na  wapenzi kupekua simu za wenza wao kwa siri,ni chanzo kikuu cha migogoro ya kifamilia inayosababisha kuvunjika kwa ndoa na uhusiano.

Kufuatia hali hiyo,Kaimu Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Magu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/Insp) Makoye Kitula, ametoa wito kwa wanandoa na wapenzi kuacha tabia ya kupekua simu za wenza wao,katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Sagani, Kata ya Kandawe, wilayani humo Mei 23,2025.

Kitula amesema,kupekua simu ya mwenza bila ridhaa yake ni uvunjaji wa haki ya faragha na ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi.

Amesisitiza umuhimu wa kuaminiana katika uhusiano,”Tuheshimiane, isifike mahali mpaka unaleta mchepuko wako nyumbani na kuuchinjia kuku,”.

Sanajari na hayo,ameonya kutoruhusiwa kupekua simu ya mwenza kisiwe kigezo cha kujiingiza katika uhusiano mpya na kuathiri familia zao.

Mkazi wa Kijiji cha Sagani, Abel Mapesa, amesema miongoni mwa mambo yanayochangia migogoro ya kifamilia ni wanawake kuwanyima waume zao unyumba na kipato duni.Ametoa wito kwa wanawake kuwajali wenza wao ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake,Ofisa Maendeleo wa Kata ya Kandawe, Aurelia Mosha, amehiasa jamii, hususani wanandoa, kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa familia.

Huku  akitoa rai kwa wanawake kutokuwa wepesi wa kutoa maamuzi ya kuwanyima unyumba waume zao pale wanapokosa kipato, kwani hali hiyo inaweza kupelekea migogoro.