March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kuwa mabalozi wa usalama barabarani

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online Igunga

WANANCHI wilayani Igunga mkoani Tabora, wamepatiwa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto.

Elimu hiyo ilioendana sambamba na zoezi la uzinduzi wa ukaguzi wa magari, leseni za udereva na vifaa vya kuzima moto ( fire extinguisher),ambayo imetolewa kituo kikuu cha mabasi Igunga na Mratibu wa Road Safety Ambassador Kanda ya Kati Zahoro Magomba, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Jeshi la Polisi Igunga kitengo cha Usalama Barabarani na Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Igunga.

Magomba amesema,mabalozi wa usalama barabarani ni wazalendo ambao wamejitoa kuisaidiana na Serikali na vyombo vyote vinavyosimamia masuala ya usafirishaji,kupaza sauti ili kutoa elimu ya  usalama barabarani, kukemea vitendo vyote ambavyo vinavunja sheria za usalama barabarani pamoja na kutoa taarifa ya matendo yote ya uvunjifu wa sheria za usalama hizo.

“Mmiliki, dereva, unayefanya kazi ya uwakala wa kusafirisha abiria na mwananchi wa kawaida, unaweza kuwa balozi wa usalama barabarani.Kwani balozi wa usalama barabarani ni mtu yoyote anayechukizwa na uvunjifu wa sheria za usalama barabarani,”.

Pia amesema, abiria wengi wamekuwa na mazoea ya kutoa historia ya ajali baada ya kutokea, hivyo amewaomba abiria wote kupaza sauti kwa kupiga vitendo vyote vinavyosababisha ajali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama barabarani.

Kwa upande wake Kamanda wa Zimamoto Wilaya ya Igunga Musa Mfutakamba, amewataka abiria kukagua chombo cha moto kabla ya kupanda,huku akiwataka madereva kuhakikisha magari yao yanana mifumo sahihi ya umeme, mlango wa dharura na kifaa cha kuzimia moto ambacho ni kizima.

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani wilaya ya Igunga SP. Joseph Mgeri,amewataka wamiliki wa vyombo vya moto na madereva kuendelea kufuata sheria zote za usalama barabarani, mawakala wa mabasi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na abiria kupaza sauti pindi wanapoona uvunjifu wa sheria barabarani.

Mwenyekiti wa kituo cha mabasi Igunga, Thom Mwakasege,amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga kuongeza taa katika kituo hicho ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi nyakati za usiku na kuongeza usalama wa abiria kwani taa zilizopo sasa ni chache.

“Pia tunaomba ufukie mashimo ndani ya kituo hiki, naamini mapato yataongezeka zaidi, lakini pia nimuombe DTO akamate maguta ya mizigo ambayo yanapakia abiria kwani yanafanya basi ndogo kutoingia kituoni kupakia abiria na kwenda kupakia nje ya kituo,”amesema Mwakasege.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga Joseph Mafuru, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wanakwenda kutenga bajeti ya kuongeza taa na kufukia maeneo yote yenye mashimo ndani ya kituo hicho.

Huku akisisitiza kuyachukulia hatua mabasi yote yanayopita katikati ya mji na kutokupita barabara inayopita katika kituo hicho.

Akizindua zoezi la ukaguzi wa mabasi katika kituo hicho mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, Ramadan Chikuve, amewataka wananchi wote waliojitokeza katika zoezi la utoaji elimu hiyo kuwa mabalozi kwa kutoa elimu waliyopatiwa, huku akimtaka DTO kuyachukulia hatua mabasi yote ambayo yanapita katikati ya makazi ya wananchi kwani maelekezo yalisha toka.